Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Royal Tour Yaitangaza Tanzania Duniani
May 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Lilian Lundo - MAELEZO

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus amesema moja ya faida ya filamu ya “The Royal Tour” ni kujulikana zaidi kwa nchi ya Tanzania duniani tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.

Zuhura amesema hayo leo, Mei 12, 2022 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini Uganda Mei 10 na 11 na ziara aliyoifanya nchini Marekani ya kuzindua filamu ya “The Royal Tour” tarehe 14 hadi 26 Aprili, 2022 kwa Waandishi wa Habari.

Zuhura amesema kuwa, faida zilizotokana na filamu ya “The Royal Tour” ni nyingi, ikiwemo kuitangaza Tanzania na kujulikana na mataifa mengin zaidi duniani, ambapo kwa sasa watu wengi wanaitazama Tanzania kupitia filamu hiyo.

“Wakati wa uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nchini Marekani takribani chaneli 350 zilishuhudia uzinduzi wa filamu hiyo. Vilevile filamu hiyo inapatikana katika mtandao wa Amazon na Apple tv ambayo inatumiwa na watu wengi dunia,” alifafanua Zuhura.

Aliendelea kusema kuwa, kulikuwa na malalamiko ya kutokujulikana wapi mlima Kilimanjaro upo, lakini kupitia filamu hiyo imeeleza vizuri kwamba mlima huo upo nchini Tanzania na sio nchi jirani. Pia, watu wengi wamefahamu kwamba madini ya Tanzanite yanapatikana nchini Tanzania peke yake na hakuna nchi nyingine inayotoa madini hayo zaidi ya Tanzania.

Kwa upande wa Mwenyeketi wa Kamati ya filamu ya Royal Tour, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa filamu hiyo itakuwa na mwendelezo wa filamu nyingine kwani waandaaji wa filamu hiyo walichukua maudhui katika maeneo mengi ya Tanzania.

“Filamu ya “The Royal Tour” inayosambaa duniani kwa sasa ina dakika 57, kwa hiyo ni saa moja. Lakini kuna maudhui ambayo yamechukuliwa na hayajatumika, ambayo ni ya zaidi ya saa 40, na ndio maana Mhe. Rais alisisitiza kwamba huko mbele, kila baada ya muda tukifanya tathmini tutakuwa tunatoa toleo lingine, kwa sababu maeneo yaliyochukuliwa ni mengi zaidi kuliko ambayo yameonyeshwa,” alifafanua Dkt. Abbasi

Aliendelea kusema kuwa, kamati imesambaza filamu hiyo kwenye televisheni zote hapa nchini ili kila Mtanzania aweze kuiona filamu hiyo. Aidha kuna toleo la filamu hiyo ambayo imewekewa nukuu za lugha ya kiswahili ili kila Mtanzania aweze kuelewa ujumbe uliokuwa unatolewa kupitia filamu hiyo.

Tanzania ni nchi ya Tisa duniani kufanya filamu ya Royal Tour, na nchi ya pili kwa bara la Afrika, ikitanguliwa na nchi ya Rwanda. Nchi nyingine ni Jordan, New Zealand, Polland, Mexico, Ecuador, Peru na Israel.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi