[caption id="attachment_8773" align="aligncenter" width="750"] Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Emmy Hudson akifafanua kuhusu zoezi la uhakiki wa vyeti kwa wanafunzi watakao omba mkopo mwaka huu (katikati). Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESBL) Bw. Abdulrazaq Badru na Afisa Usajili Muandamizi kutoka RITA, Bw. Adam Mkolabigawa (kulia).[/caption]
Agness Moshi
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wameandaa utaratibu maalumu utakaowawezesha wanafunzi wanaoomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/2018 kufanya uhakiki wa nyaraka mbalimbali kwa urahisi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mtendaji Mkuu (RITA) Bi. Emmy Hudson amesema kuwa uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo unaotumika sasa utawezesha zoezi hilo kufanyika kwa haraka na ufanisi zaidi tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambapo wanafunzi wataweza kufanya maombi ya mikopo kwa wakati.
“ Tumeandaa dawati maalum kwa wanafunzi watakao kuja kuhakiki vyeti vyao kupitia ofisi za wilaya ambazo awali zilizotoa vyeti hivyo au RITA makao makuu na kwa walio mbali na vituo hivyo wanaweza kuhakiki kupitia tovuti maalum ijulikanayo kama uhakiki@rita.go.tz” , alisema Bi.Hudson.
Ameongeza kuwa, wanafunzi watakao kwenda kufanya uhakiki wanatakiwa wahakikishe wana nakala za nyaraka zinazosomeka vizuri ikiwa ni pamoja na risiti ya malipo ambayo watalipa kupitia Benki ya NMB akaunti namba 20610009881 yenye jina la ‘Administrator General Collection Account’.
“ Ili zoezi la uhakiki kwa mwanafunzi likamilike atahitajika awe na nakala za nyaraka pamoja na risiti ya ada ya uhakiki inayolipiwa shillingi elfu tatu , utaratibu huu ni kwa wanafunzi wote hata watakaohakiki kwa kupitia tovuti” , alifafanua Bi.Hudson.
Aidha, Bi.Hudson aliwatahadharisha wanafunzi kujiepusha na udanganyifu wa aina yoyote ile kwenye zoezi hilo wakijihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka hizo watawajibishwa kwa kukiuka sheria za uombaji mikopo.
“ Kuna wanafunzi wanaua wazazi wao ili waweze kupata mikopo, huu ni udanganyifu inabidi waache kwani tutawashugulikia kwa sheria na niwataadharishe wanaotengeneza vyeti kupitia mashirika ambayo hayatambuliki kuacha hiyo tabia mara moja, mwaka jana tulibaini vyeti feki takribani 500 na tulifikisha taarifa hiyo kwenye vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua”,aliongeza Bi.Hudson.
Ametoa rai kwa wananchi ambao watoto wao wanaendelea na masomo kufanya usajili na uhakiki mapema badala ya kusubiri tukio fulani ambalo litawalazimisha kufanya shughuli hizo. Hatua hii itawasaidia kuepusha usumbufu kwao na taasisi ya RITA.
Hata Bi.Hudson amefafanua kuwa uhakiki utakaofanywa na RITA utahusisha Tanzania Bara tu na si Tanzania visiwani, aliwataka wanafunzi wa Visiwani wafanye uhakiki kupitia ofisi zilizopo Visiwani humo.
Naye , Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESBL) ,Bw.Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Bodi imefungua rasmi dirisha la uombaji mikopo kwenye tovuti zao kwa mwaka 2017/2018 tarehe 6 Agosti, na litafungwa tarehe 4, Septemba mwaka huu.
“Tumetoa mwongozo na vigezo kwa waombaji kwenye tovuti yetu ikiwa na vigezo vya mwombaji ambapo anatakiwa kuwa Mtanzania na awe ameomba kudahiliwa na Chuo Kikuu au Taasisi ya juu inayotambulika na Serikali. Aidha atatakiwa kuambatanisha vyeti vikiwemo vya taaluma, kuzaliwa na vifo ambavyo vimekwisha fanyiwa uhakiki na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA)” alisema Bw.Badru.
Aliongeza kuwa mwombaji mkopo sharti ahakikikishe ana anyaraka mbalimbali ikiwemo fomu ya maombi iliyosainiwa na Kamishna wa viapo, nakala za vyeti vya taaluma na nakala za vyeti vya kifo kama ni yatima.Endapo mwombaji alipata ufadhili anatakiwa kuwa na nakala kutoka katika taasisi iliyomfadhili.