Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

REA Kutoa Bilioni 6.7 Kujenga Mifumo ya Kupeleka Gesi Asilia Majumbani Pwani na Lindi
Dec 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umejitayaridha kutenga Shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kutengeneza mifumo ya utumiaji wa gesi asilia kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani na Lindi katika mwaka wa fedha 2023/24,

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo, Mhandisi Hassan Saidy ameyasema hayo jana katika mji wa Ifakara uliopo wilayani Kilombero mkoani Morogoro wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wa taasisi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mhandisi Saidy amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/24, REA itagawa rasilimali fedha zake kwenye sehemu mbili zikiwemo za kusambaza umeme vijijini na kusaidia upatikanaji wa nishati bora ya kupikia kwenye maeneo ya vijijini.

"Serikali inafanya kazi na taasisi binafsi na za umma kuhakikisha wananchi wanatumia nishati bora ya kupikia, sisi REA tumejipanga kushirikiana na TPDC kuanzisha mradi wa majaribio kwa mikoa ya Pwani na Lindi ambapo tutajenga mifumo ya mabomba yatakayopeleka gesi mpaka majumbani ili wananchi waanze kutumia gesi asilia ambayo inazalishwa hapa nchini na TPDC ndio wataisambaza gesi hiyo", alisema Mhandisi Saidy.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/24, REA ina mpango mwingine wa kusaidia upatikanaji wa majiko banifu takriban 200,000 kwa maeneo ya vijijini ambao utafanyika kwa ushirikiano na Benki ya Dunia. Majiko hayo yatasaidia kupunguza ukataji wa miti pamoja na kupunguza magonjwa yanayosababishwa na moshi.

Vile vile, REA inatarajia kusaidia ujenzi wa mitambo ya kuzalisha bayogesi hasa kwenye taasisi za umma na taasisi zinazotoa huduma kwa watu wnegi kwenye jamii.

Kwa upande mwingine, REA inatarajia kusambaza mitungi ya gesi takriban 100,000 kwenye maeneo mbalimbali nchini. Aidha, itaanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini kwani vituo vingi vya mafuta viko maeneo ya mijini tu.

Mkurugenzi Saidy ametoa wito kwa Watanzania kwa kila mmoja kuanza kuchukua hatua katika eneo lake kuzuia matumizi ya nishati chafu kwa kuwa ina madhara makubwa kwa afya na mazingira huku akisisitiza kuwa Serikali pia inaelekeza wananchi kuanza kutumia nishati bora na safi ya kupikia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi