Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora: Wekeni Akiba ya Chakula Kuepuka Njaa
Jul 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Tiganya Vincent, RS-Tabora

Wakazi wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kabla hawajafanya maamuzi ya kuuza mahindi yao ili kuepuka kukumbwa na njaa kutokana na upungufu wa mavuno.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri wakati wa mkutano wa viongozi mbalimbali wa Mkoa huo walipokuwa wakitathmini hali ya chakula.

Kufuatia kuwepo kwa upungufu chakula, Mkuu wa Mkoa ametoa fomu maalum kwa Wakuu wa Wilaya  na Wakurugenzi Watendaji ili mtu anayetaka kuuza chakula ajaze kabla ya kuuza kuelezea hali halisi ya chakula katika familia yake na iwapo kinachobaki kitamfikisha msimu mwingine wa mavuno.

Alisema kuwa lengo ni kutaka kudhibiti watu wanauza chakula hovyo ba baadae kuitupia lawama Seriklai pale wanapokumbwa na njaa kutokana na kuuza chakula chote.

Bw. Mwanri alisema kuwa fomu hizo zinataka atakayeu uza chakula ni yule tu mwenye ziada na sio vinginevyo.

Aliongeza kuwa ili kuepuka udanganyifu fomu hizo ni lazima zijazwe na muuzaji, mnunuzi, Mtendaji Kijiji, Mtendaji Kata na kisha nakala zipelekwe katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kama ikitokea mtu anahitaji msaada wa chakula awe ni yule ambaye hakuuza chakula.

Bw. Mwanri alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa haimzui mtu kuuza mahindi yake lakini lazima anayefanya hivyo awe ni yule mwenye ziada ambaye viongozi wameridhika kuwa kweli atabaki na chakula cha kutosha familia yake.

Aidha bw. Mwanri aliwatahadharisha wanunuzi kuhakikisha wanavyo vibali ikiwemo fomu hiyo maalum kabla ya kusafirisha mahindi yao kutoka eneo moja kwenda jingine ili kuepuka usumbufu.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara alisema kuwa mahitaji ya Mkoa huo toka msimu moja wa mavuno hadi mwingine ni tani 605,864 za nafaka aina ya mahindi, lakini mavuno ya mwaka huu ni tani 445,362 ikiwa ni pungufu ya tani 160,502. za mahindi.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wananchi wanatakiwa kabla ya kuuza chakula chao ni vema wakajihakikishia kuwa na ziada ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia zao kwa kipindi chote hadi mavuno mengine.

Dkt. Ntara alitoa wito kwa wakazi wa Tabora ambao hawakupata mavuno mazuri kutumia muda huu kununua kwa wingi chakula kwa ajili ya kujiwekea akiba kwa kuwa bei bado iko chini.

Mkoa wa Tabora walipata mvua kwa kipindi cha miezi miwili tu kitu kilichosababisha baadhi ya mazao kushindwa kukomaa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi