Na Tiganya Vincent - RS Tabora
SERIKALI imewaonya Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika Mkoani Tabora ambao wanafikiri wanaweza kugeuza Ushirika kuwa maficho ya kuwanyonya wakulima kuondoka mara moja kabla ya hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 22 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ingembensabo.
Alisema kiongozi aliye madarakani ajipime kama ni safi na mwadilifu na sio kuwa kama kibaka mzoefu.
Mwanri aliongeza kuwa watu wanaofanya ujanja ujanja kwa ajili ya kutaka kuwanyonya wakulima wawachukulie hatua mapema kabla ya mambo hayajaharibika.
Alisisitiza kuwa kila kiongozi ajifikirie moyoni mwake kama kweli anaweza kuwa msafi ndio awe kiongozi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema maelekezo ya serikali ni kwamba pamba yote itauzwa kupitia ushirika na sio vinginevyo kwa kuwa lengo ni kutaka mkulima asinyonywe.
Alisema ushirika ndio njia pekee inayowashika mkono wakulima wanyonge.
Naye Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Tito Haule alisema kuwa kiongozi yoyote aliyewania uongozi kwa ajili ya maslahi binafsi ni vema ajiondoe mapema katika Ushirika ili asije akajikuta sehemu mbaya.
Alisema kiongozi atakayekutwa akiwa amegeuza Ushirika kama sehemu ya kupatia fedha kinyume cha Sheria atakamatwa na hataachiwa na atashitakiwa kama mhujumu uchumi.
Aidha Haule aliwataka viongozi wa Ushirika kutoishia katika kukaa Ofisini bali nao walime pamba ili wakulima wengine waende kujifunza jinsi ya kulima vizuri.