Na Tiganya Vincent, Nzega
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amesema kuwa atawachukulia hatua ikiwemo kuwapeleka katika Mamlaka zao za uteuzi viongozi na Madiwani ambao wamekuwa wakijitokeza kuwatetea watumishi waliosimamishwa au kufukuzwa kwa makosa mbalimbali kama vile ubadhirifu wa mali za umma .
Mwanri alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Tabora yaliyofanyika wilayani Nzega kuhusu jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi jamii ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) iliyoboreshwa na usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo (LGDG)
Alisema kuwa imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo mtumishi anakuwa ametuhumiwa kwa makosa mbalimbali na kusimamishwa ili kupisha uchunguzi tuhuma zake kunajitokeza baadhi ya madiwani au viongozi kujifanya wao ni watetezi wake bila kujali hasara iliyotokana na utendaji wake na utovu wa nidhamu.
Mwanri alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya Halmashauri kwa sababu ya baadhi ya Madiwani au viongozi fulani kuwa na maslahi binafsi na mtuhumiwa kwa sababu wanaona kuwa kutokuwepo kwake ni pigo kwao.
Alisisitiza kuwa somo la wajibu na maadili walilofundishwa linawataka kuhakikisha kuwa wanakuwa wazalendo kwa kulinda maslahi ya wananchi na sio kikundi fulani cha waharifu au wezi.
“Nikimsikia mtu anamtetea mtumishi aliyefukuzwa au kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu naanza nay eye kama yuko katika uwezo wangu nitamdoa na yeye ili akamtetee vizuri akiwa nje …na kama ni Diwani nitampeleka katika Chama chake kwa kuwa ndio kilichompa dhamana ya kwenda kwa wananchi kuomba kura ili aweze kuchukuliwa hatua kwa sababu ya kuwasaliti wananchi waliomchagua” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aliwataka Madiwani wawe na uchungu na wananchi kwanza na kuacha kutetea maovu katika Halmashauri zao kama wanahitaji maendeleo ya watu wao yaonekana na majina yao yawekwe kwenye Historia nzuri na sio ile ya kudharauliwa hata na vijana wadogo.
Naye Afisa Utumishi , Ofisi ya Rais-TAMISEMI Debora Mkemwa akitoa mada kuhusu nidhamu kwa watumishi na mashauri ya nidhamu kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa alisema kuwa uchunguzi wa awali unafanyika kabla ya hatua za kinadhamu kwa mtumishi hazijachukuliwa ili kujiridhisha iwapo zipo sababu za msingi za kuanzishwa mchakato huo.