Na Tiganya Vincent, NZEGA
Madiwani katika Halmashauri za Mkoa wa Tabora wametakiwa kuepuka kujenga makundi miongoni mwao ambayo yamekuwa yakisababisha wananchi waliowachagua kuchelewa kupata maendeleo kwa sababu ya muda mwingi kushughulikia migogoro badala ya kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Tabora yaliyofanyika wilayani Nzega kuhusu jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi jamii ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) iliyoboreshwa na usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo (LGDG)
Alisema makundi yatawafanya washindwe kuwajibika vizuri na kujikuta miaka mitano ya uongozi wao inakwisha bila kuwafanyia chochote wananachi zaidi ya kupigania kuondoana katika uongozi badala kukazania maslahi ya wananchi.
“Nyie ndio mliko zamu sasa mkiendekeza makundi na migogoro isiyokwisha, mtajikuta zamu zenu zinamalizika hamjawafanyia chochote wananchi waliowachagua badala yake kupambana kila mnapokutana katika vikao vyenu ….kila kikao itakuwa sisi hatumutaki fulani atuongoze au fulani fulani hatufai” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Bw. Mwanri aliongeza kuwa wakimruhusu Shetani wa namna hiyo apite kati yao hakuna tena kazi wala maendeleo kwa wananchi wao waliowachagua.
Alisisitiza kuwa viongozi wa aina hiyo wanakuwa wamekosa sifa ya kuendelea kuaminiwa na jamiii iliyowachagua tena kuwatetea wananchi katika matatizo yanayokwamisha maendeleo yao.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Madiwani wote washirikiane bila kujali itikadi za vyama vyao, dini zao, kabila zao katika kuhakikisha kuwa wanatetea vyema wananchi wao na wanasimamia vyema watendaji wa Halmashauri zao kwa ajili ya kuwaletea wananchi maisha bora.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Leopold Chundu Ulaya alisema kuwa mafunzo walipatiwa na wawezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na TAMISEMI yatawasaidia kuhakikisha kuwa miradi yote inatekezwa kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Alisema kuwa watajitahidi kuunganisha nguvu kwa pamoja kwa kubadilika ili kuhakikisha kuwa wanatatua matatizo ya wananchi waliowachagua na kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.