Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora Amtaka Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Kuongeza Bei ya Pamba
Jul 27, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Tiganya Vincent-RS TABORA

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Aggrey Mwanri amemtaka Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kupandisha bei ya kununua pamba kutoka shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa kilo ili kuwavutia wakulima wengi kuuza bidhaa hiyo katika kiwanda hicho na kuwa na malighafi ya kutosha.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora alitoa kauli hiyo leo Mjini Tabora wakati walipoongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kutembelea kutembelea Kiwanda hicho ili kuangalia halisi ya kiwanda na kutoa ushauri wa kuboresha utendaji kazi.

Bw. Mwanri aliongeza kuwa upatikanaji wa pamba kwa wingi kwa ajili ya kiwanda hicho na uzalishaji wa nyuzi na kamba ambazo zina viwango bora utawasaidia  wao kiwanda hicho ushindani katika masoko mbalimbali na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya Serikali.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amemtaka Mmiliki wa Kiwanda hicho kupeleka nakala ya Mkataba uliosainiwa wakati wa Ubinafishaji ili kuona kama anazingatia masharti ya ununuzi wa kiwanda hicho.

Aliongeza kuwa upo uwezekano wa kuwepo maeneo ambavyo yapo katika mkataba huo lakini bado mnunuzi huyo hajatekeleza na ndio sababu ya kususua kwa kiwanda hicho.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora,k Urveshi Rajani alisema kuwa yuko tayari kununua pamba yote ya wakulima wa Mkoa wa Tabora endapo atahakikishiwa upatikanaji wa soko la bidhaa zao kama nyuzi, ikiwemo wakulima wa tumbaku kupitia Chama cha Ushiriki cha Wakulima wa Tumbaku(WETCU) kununua.

Alisema kuwa kama WETCU wataamua kununua nyuzi zao wako tayari kuhakikisha wananunua pamba yote inayolimwa mkoani Tabora kwa bei nzuri na kuendelea kuboresha bei kulingana na wanavyouza bidhaa zao.

Aidha Mkurugenzi huyo Mtendaji alitoa wito kwa Serikali kudhibiti uuingazaji kinyemela wa bidhaa kutoka nje kama vile Khanga ambazo zinazalishwa nje lakini zinaandikwa kuwa zimetengezwa Tanzania, hali inayochangia kudhofisha Viwanda nchini.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara alitoa wito Watendaji wote kuhakikisha wanasimamia wakulima wanazalishe pamba ya nyingi kwa ajili ya kukiwezesha kiwanda hicho kuwa na malighafi ya kutosha ili kuzalisha nyuzi za kutoa.

Aliongeza kuwa wanapaswa kuwasimamia wakulima ili wazalishe pamba ambayo itakuwa safi na itamvutia Mmiliki wa Kiwanda hicho kununua kwa wingi na kutoa bei ya juu zaidi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Queen Mlozi alitoa wito kwa wazalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo tumbaku, korosho na kahawa kununua nyuzi za Kiwanda cha Tabora ili kuunga mkono juhudi za Mwekezaji huyo na kumsaidia ili uzalishaji wake utakapoongezeka atatoa ajira kwa vijana wengi.

Kiwanda cha Nyuzi Tabora hivi sasa kina watumishi 24 tu badala ya 350 waliokuwepo hapo awali.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi