Na: Tiganya Vincent, RS Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewaagiza viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi(AMCOS) kuhakikisha vinatenga sehemu ya mapato vitakayopata msimu huu wa mauzo ya tumbaku na pamba kwa ajili ya kununulia matrekta.
Hatua hiyo inalenga kuleta mapinduzi ya kilimo miongoni mwa wakulima ambao ni wanachama wao na wale ambao sio wanachama.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana katika Wilaya ya Kaliua na Urambo alipokutana na wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa vijiji, Kata , Maafisa Elimu Kata na walimu wakuu.
Alisema matumizi wa mashine kama vile matrekta katika kilimo ndiyo yatakayowezesha wakulima mkoani humo kupiga hatua na kupata ziada itakayotumika kuwaletea maendeleo na hivyo kuwa na malighafi nyingini kwa ajili ya viwanda na matumizi mengine.
“Tunataka kila Chama cha Ushirika cha Msingi kwa kutumia ile sehemu ya pesa kinachopata kwa kila kilo inayouzwa kinunue trekta ili tuondokane na matumizi ya jembe la mkono ambalo kwa kiasi kikubwa halitoi uwezo kwa mkulima kulima eneo kubwa katika muda mfupi ambapo mavuno yake ndio yangempa ziada” alisema Mwanri.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema trekta hilo linaweza kutumika kama chanzo cha mapato kwa Chama cha Msingi kuwakodishia wanachama wake na wasio wanachama wake wakati wa kulima na wakati wa kusomba mazao mbalimbali kutoka mashambali.
Mwanri aliongeza kuwa kilimo kitakapo kuwa cha kisasa na kilichochukua eneo kubwa wakulima wataanza kufikia hata kutumia mashine kubwa katika uvunaji wa mazao yao mbalimbali.
Alisema sanjari na hilo ameagiza kuanzia sasa kila zao linalolimwa Mkoani Tabora ni lazima lilimwe kwa kufuata mstari na pia mkulima atumie mbolea za viwandani au samadi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri katika uzalishaji.