Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Rukwa Azuia Tani 2,143 za Madini ya ‘Clinker’ Kusafirshwa Nje ya Nchi
Aug 26, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu, Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelote Stephen amezuia kusafirishwa nje ya nchi tani 2,143 za madini aina ya “Clinker” yanayotumika katika kuzalishaji saruji.

Zuio hilo amelitoa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Kasanga iliyopo katika ziwa Tanganyika huko Wilayani Kalambo jirani na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Usafirishaji wa madini hayo umekuwa ukifanywa na kampuni ya Mbeya Cement ya jijini Mbeya tangu mwezi wa Februari mwaka huu kwenda nchini Burundi kwa kampuni ya kutengeneza saruji ya Burundi Cement iliyopo jijini Bujumbura.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema ameweka zuio hilo hadi hapo atakapojiridhisha na utaratibu mzima wa usafirishwaji na uuzwaji wa madini hayo.

Hadi kuzuiwa usafirishaji huo, tayari tani 4,760 zilikuwa zimesafarishwa ambapo tani moja iliuzwa kwa dola za kimarekani 128.

Katika ukaguzi wake huo, Mkuu wa Mkoa aligunduliwa kuwa kampuni hiyo ya Mbeya Cement ina shehena ya tani 2,050 ya mifuko ya saruji bandarini hapo tangu mwezi Novemba mwaka jana na alipoulizwa mwakilishi wa Kampuni hiyo Sabas Sokoni alijibu kuwa Saruji hiyo imekosa wateja.

“Sisi tunajuwa kwamba bandari hii inapokea simenti na kuuzwa nchi za jirani… haya ni madini. Haiwezekani tukadanganya kwamba tunapeleka madini kumbe tunapeleka “raw materials” (maligafi) kutoka Tanzania kwa ajili ya kutengeneza simenti” alisema Mkuu wa Mkoa na kusisitiza kuwa “kila siku tunazungumza suala la kuongeza thamani ya vitu vyetu ili tuuze “finished products” na sio “raw materilas.”

Alifafanua kuwa utaratibu uliopo ni kwamba saruji inazalishwa Tanzania na kuuzwa nje ya nchi na sio kusafirisha udongo wa kutengenezea simenti na kuhoji kwanini udongo huo uwe na soko zaidi kuliko simenti yenyewe.

Wakati anatoa zuio hilo tani 800 za madini hayo zilikuwa tayari zimepakiwa kwenye meli ya MV Tora yenye namba za usajili BY 0064 inayopeperusha bendera ya Burundi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi