Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Lindi Awaombea Mikopo Wakulima
Aug 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu, Lindi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwakopesha wakulima wa mazao ya Muhogo na ufuta na ili waweze kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara.

RC Zambi alitoa wito huo wakati wa mkutano wa Wadau wa Korosho na Ufuta Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Bw. Zambi alisema kuwa mkoa wa Lindi ni mkoa uliojaaliwa katika kuzalisha mazao ya mihogo na ufuta lakini changamoto kubwa ni mtaji wa kulima kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

“Wakulima wa mkoa wa Lindi wapo tayari kushiriki katika kuleta mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara lakini kwa sasa suala la mtaji wa kilimo cha kibiashara ni changamoto kubwa,” alisema Bw. Zambi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema kuwa Benki ya kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo waliokuwa kwenye vikundi ili waweze kukopeshwa.

Bw. Assenga aliongeza kuwa Benki ya Kilimo pia ipo tayari kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa kuipatia mikopo yenye riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko.

“Kwa kutambua umuhimu wa wakulima wadogo wadogo nchini TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi yenye tija katika sekta ya kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” alisema.

Naye, Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema kuwa TADB inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma zisizo za kifedha kwa wakulima kama vile kujengewa uwezo juu ya uandaaji wa andiko la miradi ya kilimo, pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko, usimamizi wa biashara, mafunzo juu ya miradi ya kilimo na mbinu za majadiliano ya mikataba.

“Tupo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo,” alisema.

Bw. Chacha aliongeza kuwa kwa upande wa mikoa ya kusini Benki ya Kilimo imejipanga kueendeleza miundombinu ya umwagiliaji na maghala pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo na kuimarisha viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta, mihogo.

Bw. Chacha aliongeza kuwa Benki imejipanga kuwezesha uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya mihogo, korosho na ufuta mkoani Lindi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi