Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Afunga Maduka kwa Kuuza Bidhaa Hatarishi
Jun 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent-RS TABORA

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri ameongoza zoezi la ukaguzi wa maduka ya dawa na chakula na kufunga mawili baada ya kubainika kuuza chakula katika mazingira machafu na lingine vipodozi na sabuni zilizopigwa marufuku nchini.

Bw. Mwanri kwa kushirikiana na Maafisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), ametekeleza zoezi hilo la kushitukiza jana kwenye Mtaa wa Ujiji kata ya Gongoni katika Manispaa ya Tabora.

Alisema kuwa yeye na (TFDA) wana dhamana ya kuhakikisha wakazi wote wa Mkoa huo wanakula chakula ambacho hakihatarishi maisha yao na kutumia vipodozi ambavyo havina kemikali.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa vipodozi vyenye viambata vyenye sumu vilivyokamatwa katika duka la vipodozi, vitaorodheshwa ili vijulikane kwa ajili ya kuanda taratibu za kumshitaki mhusika na hatimaye kuteketezwa kabisa.

Aliwaagiza Maafisa wa TFDA kuhakikisha vipodozi na sabuni zenye sumu zilizokamatwa hazitoroshwi na kama wataona wanahitaji msaada wa Polisi wamweleze ili bidhaa zote zisizofaa zichukuliwe.

Katika ukaguzi mwingine Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika kufunga duka la chakula la mfanyabiashara mmoja kwa kosa la kuweka bidhaa za kula binadamu katika mazingira machafu ambayo yanahatarisha maisha ya watumiaji.

Alisema kuwa sehemu ya kuuzia chakula ni sharti iwekwe katika mazingira ambayo ni safi  na salama kwa mtu anayetumia bidhaa hiyo ili kulinda afya yake.

Kwa upande wa Meneja wa Kanda ya Magharibi wa TFDA Dkt. Edgar Mahundi alisema kuwa bidhaa zilizokamatwa zinatarajiwa kuteketeza mara baada ya wahusika kufikishwa Mahakamani na chombo hicho kutoa uamuzi.

Alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha kabla ya kunua bidhaa wanaangalia kama haijaisha muda wa matumizi na pia kama haikuwa katika orodha ya bidhaa zilizopigwa marufuku.

Meneja huyo wa Kanda alisema kuwa sasa wanatarajia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara kwa sababu bado wafanyabiashara wanauza bidhaa zilizopigwa marufuku.

Dkt. Mahundi alitoa wito kwa wananchi kusaidia kuwafichua watu wote wenye tabia ya kuuza bidhaa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi