Timu ya wataalamu waliochaguliwa kuziwakilisha idara na vitengo mbalimbali kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imewasilisha rasmi Rasimu ya Mpango Mkakati (Strategic Plan 2025/26 - 2030/31) kwa Menejimenti ya TANAPA leo Februari 04, 2026 jijini Dodoma ili kuweka maoni yao yaweze kujumuishwa katika Mpango Mkakati huo unaotarajiwa kuanza kutumika Julai Mosi, 2026 na kuendelea hadi Juni 31, 2031.
Mpango Mkakati huo utaakisi mwelekeo wa kimkakati uliobeba maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, vipaumbele vya kitaifa, malengo ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na malengo ya TANAPA ili kuongeza uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali na utoaji wa huduma wenye tija kwa wadau mbalimbali wakiwemo watalii, wawekezaji, watoa huduma na wafadhili katika masuala ya uhifadhi.
Akitoa tathmini ya zoezi zima kwa Menejimenti ya TANAPA iliyoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Sekela Mwangota, Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini - (TANAPA) ambaye ni Msimamizi Mkuu wa maandalizi ya Mpango Mkakati huo alisema;

“Hatua ulipofikia Mpango Mkakati huu ni nzuri na tutawapitisha kila hatua ili tupate maoni yenu ambayo nayo ni muhimu kuyaingiza ili tupate dira itakayokidhi malengo ya taasisi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo”.
Aidha, Kamishna Sekela aliongeza kuwa Mpango Mkakati huu umebeba vipaumbele vingi mojawapo ni kuweka nguvu katika kufufua Shoroba za wanyamapori (corridors) mbili zinazoelekea kupotea kutokana na uvamizi wa wananchi kusaka makazi, kilimo na changamoto ya mabadiliko ya Tabianchi ili kuruhusu wanyamapori kutumia njia zao za asili kusaka malisho na maji kwa nyakati mbalimbali, hatua hii inaweza kupunguza athari za migogoro kati ya wanyamapori na binadamu.

Akifungua kikao hicho kabla ya wasilisho la Mpango Mkakati huo, Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji alipongeza juhudi za timu ya wataalamu hao kwa maandalizi na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia mapendekezo yatakayoboresha zaidi rasimu hiyo kabla ya kuidhinishwa na Bodi ya Wadhamini TANAPA na hatimaye kutekelezwa rasmi kuanzia Julai Mosi, 2026.

Akiwasilisha Mpango Mkakati huo, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Wilhelm Kiwango ambaye ni mwezeshaji katika Mpango Mkakati huo alisema; “Uandaaji wa Mpango Mkakati huu umetokana na tathmini ya utendaji kazi wa Mpango Mkakati uliopita 2020/21 - 2025/26, uchambuzi wa Mazingira ya ndani na nje, mahitaji na matarajio ya Wadau mbalimbali, hivyo tuna matumaini makubwa kuwa mkakati huu utakuwa nyenzo na dira ya kufikia malengo saba yaliyoainishwa.”
Dkt. Kiwango aliongeza kuwa mambo mengi yameangaziwa katika Mpango Mkakati huu, likiwemo suala la mimea vamizi. Kwa tathmini zilizofanyika kuna aina takribani 160 zilizogundulika ambazo zimeendelea kuathiri ikolojia ya Hifadhi za Taifa nchini, hivyo mpango huu umeweka miongozo mbalimbali ya kukabiliana nayo ili kupunguza madhila yake kwa wanyamapori na mimea mingine ya asili.

Hata hivyo baada ya wasilisho michango mbalimbali kutoka kwa Makamishna, Wakuu wa idara na vitengo walipata wasaa wa kuchangia, kutoa maoni na ushauri, ambapo timu ya wataalamu hao ikiongozwa na Kamishna Sekela ambao ndio waandaaji wa Mpango Mkakati huo walikubali kuyachukua na kuyajumuisha katika Mpango Mkakati huo wa 2025/2026 - 2030/2031.