Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RAS Iringa Aitaka NEMC Kuutazama Mto Ruaha kwa Jicho la Kipekee
Jul 19, 2023
RAS Iringa Aitaka NEMC Kuutazama Mto Ruaha kwa Jicho la Kipekee
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Leonard Masanja akiwa katika picha ya pamoja na timu ya Watumishi wa NEMC - Kanda ya Kati walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha ambapo kwa sasa Mkoa huo unahudumiwa na NEMC Kanda ya kati badala ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kama ilivyokuwa awali.
Na Tajiri Kihemba- NEMC Kanda ya Kati

Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Leonard Masanja amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza nguvu katika kuulinda mto Ruaha.

Mhandisi Masanja ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na timu ya Watumishi wa NEMC - Kanda ya Kati walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha ambapo kwa sasa Mkoa huo unahudumiwa na NEMC Kanda ya kati badala ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kama ilivyokuwa awali.

“Uhifadhi wa vyanzo vya maji ukiwemo mto Ruaha unaopita katika mbuga ya wanyama ni eneo ambalo linatakiwa liangaliwe kwa jicho la kipekee sana” Alisema Mhandisi Masanja.

Akizungumzia kuhusiana na uharibifu unaoendelea wa vyanzo vya maji amesema, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ipo na inabidi kusimamiwa.

“Tuna vyanzo mbalimbali vya maji katika mkoa wetu wa Iringa lakini kutokana na ukame unaojitokeza watu huvamia maeneo ya vyanzo hivyo vya maji, kuna sheria inayoelekeza shughuli zote zifanyike umbali wa mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji, hivyo ni vizuri kuisimamia”, aliongeza Mhandisi Masanja.

Naye, Afisa Mazingira wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Golyama Bahati alisema kuwa kwa mwaka 2023 mkoa huo umefanya vizuri katika upandaji miti ambapo jumla ya miti milioni 35 imepandwa hadi kufikia mwezi Julai 2023.

“Kwa mwaka huu 2023, Iringa tumepanda miti milioni 38, ni tofauti na mwaka jana na juzi ambapo tulikuwa tunaishia kupanda miti milioni 35, kwa hiyo suala la kupanda miti ni utamaduni wetu”, alieleza Dkt. Golyama.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kati NEMC, Dkt. Careen Kahangwa ametumia fursa hii kuwakumbusha Watanzania kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwani ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anatunza mazingira ili kulinda afya yake na ya jamii inayomzunguka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi