Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba utayari wa Uholanzi kuunga mkono mikakati pamoja na Sera ya uchumi wa Buluu kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyowekwa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Zanzibar katika mazunguzo kati yake na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Wiebe de Boer.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya Uholanzi kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo uchumi ambapo nchi hiyo tayari imepiga hatua katika miongoni mwa sekta hizo.
Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Balozi Wiebe de Boer namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha na kuuendeleza uchumi wa Buluu huku akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuja kuwekeza Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alimuahidi Balozi Wiebe de Boer kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji watakaoamua kuja kuwekeza Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Uholanzi na kusisitiza haja ya kuongeza ushirikiano huo hasa katika sekta mbali mbali za maendeleo ukiwemo Uchumi wa Buluu.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Balozi huyo namna mikakati ilivyowekwa katika kuimarisha sekta nyengine za uchumi ikiwemo kilimo cha mwani na juhudi zinazochukuliwa katika kukiimarisha pamoja na sekta ya uvuvi ambapo Zanzibar inataka iondokane na uvuvi unaofanyika hivi sasa kutokana na kutokuwa na tija wala kipato kwa wavuvi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Nae Balozi wa Uholazi nchini Tanzania, Wiebe de Boer alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba Uholanzi imekuwa na uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar tokea miaka ya 60 na kusisitiza haja ya kuimarishwa.
Balozi Wiebe de Boer alimuahidi Rais Dkt. Mwinyi kwamba Uholanzi iko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika kutimiza kiu yake ya kuimarisha uchumi kupitia uchumi wa Buluu.
Alieleza kwamba kwa vile nchi hiyo tayari imepiga hatua kubwa katika sekta za uchumi wa Buluu hivyo itahakikisha inaiunga mkono Zanzibar ili nayo ifike pale ilipokusudia ikiwa ni pamoja na kuzishawishi Kampuni kadhaa za nchi hiyo pamoja na wawekezaji kuja kuangalia mazingira ya uwekezaji ya Zanzibar.
Balozi huyo pia, alimueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua atakazozichukua katika kuhakikisha anaitangaza vyema Zanzibar kiutalii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunaandaliwa mazingira mazuri ya usafiri wa watalii kutoka nchi hiyo moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika makubwa ya ndege ya nchi hiyo.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa UN WOMEN Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Maxime Houinato akiwa amefuatana na ujumbe wake alifika Ikulu Zanzibar kuzungumza na Rais Dkt. Mwinyi ambapo alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa jinsi anavyozingatia suala zima la usawa wa kijinsia katika uteuzi wake wa viongozi.
Mkurugenzi huyo pia, aliahidi kwamba UN WOMEN itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mikakati yake ya kuwaunga mkono wanawake katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Nae Rais Dkt. Mwinyi kwa upande wake alimuelezea kiongozi huyo mikakati mbali mbali iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakaikisha wanawake na watoto wanapata haki zao za msingi.
Aidha, alieleza hatua zilizowekwa na serikali anayoiongoza katika kuwawezesha wanawake.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.