Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais wa Misri Kuwasili Nchini Wiki Ijayo
Aug 11, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_8905" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi. Dkt. Aziz Mlima akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam juu ya ziara ya Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah Al Sisi inayotarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo. (Picha na Thobia Robert-MAELEZO)
[/caption]

Thobias Robert-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Abdel Fattah Al Sisi anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania kufuatia mwaliko wa Rais John Pombe Magufuli alioutoa mwanzoni mwa mwaka huu.

Ziara hiyo itakuwa ya kwanza nchini kwa Rais wa nchi hiyo ambayo ni ya pili kwa uchumi mkubwa barani Afrika na ya kwanza tangu Rais John Magufuli alipoingia maradakani Oktoba mwaka 2015.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz Mlima amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha na kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Tanzania na Misri tumekuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri kwa miaka mingi tangu wakati wa waasisi wa nchi zetu Mwalimu Julius Nyerere na Jamal Abdel Nasser hivyo ziara ya Rais Al Sisi ni kukuza uhusiano wetu huo” Dkt. Mlima alieleza.

[caption id="attachment_8908" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi. Dkt. Aziz Mlima akiwaeleza Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam juu ya ziara ya Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah Al Sisi inayotarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo. (Picha na Thobia Robert-MAELEZO)[/caption]

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, akiwa nchini, Rais wa Misri atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli ambayo yatafuatiwa na mazungumzo rasmi ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Alifafanu kuwa chini ya uhusiano huo nchi mbili zimekuwa zikishirikiana katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiulinzi pamoja na medani za siasa za ushirikiano wa kimataifa, kutetea haki za binadamu pamoja na kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika.

Aliyataja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni pamoja na mawasiliano, usafiri, ulinzi, na usalama pamoja na ushirikiano wa kimataifa.

Aidha, Katibu Mkuu Mlima alibainisha kuwa, nchi hizi zimekuwa zikishirikiana katika ngazi za kitaasisi za Kiserikali kama vile Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri (Administration Control Authority of Egypt) ambayo imekuwa ikishirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa ya Tanzania (TAKUKURU).

Aliongeza kuwa kuna ushirikiano mzuri kati ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri ambavyo vinashirikiana kwa kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa shahada za juu za uzamili na uzamivu.

Zaidi, Balozi Dk. Mlima aliwaeleza Waandishi wa Habari kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) wamesaini makubaliano ya ushirikiakiano na Kampuni ya Polyserve ya nchini Misri.

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa ujumbe wa Rais wa Misri utajumuisha pia wafanyabiashara ili kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo ambapo alisema nchi hiyo ni moja ya nchi zinazowekeza nchini.

“Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji (TIC) uwekezaji kutoka nchini Misri kati ya mwaka 1990 hadi 2017, unaonesha kuwa wawekezaji toka nchi hiyo wamewekeza katika miradi nane yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 887.2 na kutoa ajira zipatazo 953”, alisema Balozi Mlima na kufafanua kuwa uwekezaji huo umefanywa katika maeneo ya kilimo, viwanda (Mbolea, madini, dhahabu, na shaba) na sekta ya huduma.

Tanzania na Misri zina mahusiano mazuri ya kidplomasia ya muda mrefu ambayo yameasisiwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo ambao ni Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Kiongozi mashuhuri wa Taifa la Misri Hayati Gamal Abdel Nasser.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi