Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia: Tunajenga Barabara Kuifungua Nchi Kiuchumi
Feb 26, 2025
Rais Samia: Tunajenga Barabara Kuifungua Nchi Kiuchumi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Pangani -Tanga (km 256) sehemu ya Mkange-Pangani-Tanga (170.8) pamoja na Daraja la mto Pangani (M525) kwenye hafla iliyofanyika Pangani mkoani Tanga tarehe 26 Februari, 2025.
Na Grace Semfuko - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake imeamua kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuifungua nchi kiuchumi, ambapo kupitia miundombinu hiyo, wananchi watapata fursa ya kufanya biashara kwa urahisi.

Amesema daraja la mto Pangani lililopo wilaya ya Pangani mkoani Tanga, litakuwa kiunganishi kati ya baadhi ya mikoa nchini Tanzania, pamoja na nchi jirani ya Kenya kupitia Mombasa.

Rais Samia amesema hayo leo February 26, 2025, wakati akizungumza na wwananchi wa wilaya ya Pangani, mara baada ya kuzindua boti za uvuvi, kilimo cha mwani pamoja na kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa daraja la mto Pangani na barabara ya Bagamoyo kupitia Makurunge-Saadani hadi Tanga yenye urefu wa kilomita 256.

"Kwa nini tumejenga miundombinu hii, ni kwa sababu tunataka uchumi wa Pangani ubadilike, lakini pia tuna dhamira ya kuiunganisha Tanga na shoroba kadhaa na kanda kadhaa za kiuchumi. Tukiangalia daraja lile linaunganisha toka Bagamoyo hadi mpaka wetu na Kenya, sasa kule Bagamoyo tunakwenda kujenga eneo huru la kiuchumi, tunakwenda kujenga kongani la viwanda pale Bagamoyo (EPZA) kubwa kuliko zote Tanzania" amesema Rais Samia.

Amesema pia Serikali itajenga Bandari ya Bagamoyo, hivyo Tanga inaunganishwa na Bagamoyo kwenye eneo kubwa la uhuru wa kiuchumi na bandari kubwa.

Fauka ya hayo, Mheshimiwa Rais amesema wilaya ya Pangani inaunganishwa na wilaya kadhaa hadi kufika Mombasa nchini Kenya ambapo huko na wao wanaimarisha miundombinu hiyo kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi kupitia usafirishaji.

"Kwa hiyo huu ni ushoroba mkubwa kiuchumi, lakini barabara hii tunayoiunganisha inakwenda kuifungua Tanga kiutalii na kibiashara pia, maeneo kadhaa ya Tanga ambayo hayafikiki kiurahisi kwa utalii sasa yatafikika" ameeleza Rais Samia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi