Na Mawazo Kibamba - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inahitaji viwanja vitatu vya mpira vya ziada kati ya vitatu ilivyonavyo ili kukidhi vigezo vya kuwa na ushindani wa kushiriki Fainali za Michuano ya Klabu Bingwa Afrika-AFCON.
Amesema mahitaji ni kuwa na viwanja sita vinavyotambulika kisheria ambapo kwa sasa vipo vitatu tu vikiwepo vya Mkapa, Uhuru vya Dar es Salaam na cha Amani kilichopo Zanzibar.
Ameyasema hayo leo Mei 31, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akipokea Kombe la Dunia la mashindano ya mpira wa miguu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kombe la Dunia ya mpira huo yanayotarajia kufanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 21, 2022 hadi Desemba 18, 2022 yatakayoshirikisha mataifa 32.
"Ili tufanye mashindano ya AFCON inabidi tuwe na namba (idadi) kadhaa ya viwanja vya soka, nadhani mahitaji ni viwanja sita, sasa hivi tuna viwanja vinavyotambulika vitatu tu, viwanja vyetu vya hapa Dar es Salaam, lakini Zanzibar na kimoja cha Amani, kwa hiyo tunahitaji viwanja vitatu vingine vyenye sifa ndipo tutaweza kufanya mashindano hayo hapa kwetu Tanzania, kila mtu akiwajibika tunaweza kufanya mashindano haya hapa, kwa upande wetu tutakwenda mbio kushawishi kila tunaemuweza atusaidie kwenye ujenzi wa viwanja, tukitimiza viwanja vitatu, tukitimiza aina ya hoteli zinazotakiwa, aina ya usafiri unaotakiwa, mashindano kwa mara ya kwanza yatafanyika hapa” amesema Rais Samia.
Ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wa soka nchini, kushirikiana katika kuleta hamasa kwa vijana kujiandaa katika kushiriki kwenye michuano ya kimataifa ya mchezo wa soka.
"Kombe la dunia kuletwa hapa kwetu ni uamsho na wito kwa vijana wetu, kuwatayarisha vizuri zaidi, sasa hivi tumeambiwa kuwa timu zetu za wanawake zinakwenda vizuri sana, timu zetu za wadogo wadogo zinakwenda vizuri sana, lakini hatumalizii vizuri sana. Kombe hili mlitupe uamsho, kuwatayarisha watoto wetu vizuri zaidi ili waweze kufanya vizuri zaidi si kwa kutetema na kunyunyiza lakini kwa ufundi na akili, tujitahidi sana” amesema Rais Samia.
Nae Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania imepata heshima kupewa nafasi kubwa Duniani kuwa ni miongoni mwa mataifa tisa Barani Afrika ambayo yanatembelewa na Kombe la Dunia la mwaka huu wa 2022, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kombe la Dunia ya mpira wa miguu yanayotarajia kufanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 21, 2022 hadi Desemba 18, 2022 yatakayoshirikisha mataifa 32
"Mheshimiwa Rais historia ya mashindano haya yalianza tangu mwaka 1930 na kufanyika kwa mara ya kwanza nchini Uruguay chini ya usimamizi ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), michuano hiyo inafanyika kila baada ya miaka minne, Mheshimiwa Rais ni Mkakati wa Wizara wa kushirikiana na wenzetu wa mpira wa miguu la nchini Tanzania (TFF) katika kuhakikisha kuwa tunaandaa timu yetu ya Taifa ya Tanzania ili kushiriki katika fainali za michuano ya klabu bingwa Afrika-AFCON za mwaka 2027, tumedhamiria, tayari chakatao unaendelea kwa ajili ya kusaka vipaji vya vijana kupitia program ya mtaa kwa mtaa inaendelea” amesema Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka FIFA Bw. Juliano Haus Belletti amesema ujio wa kombe la Dunia nchini Tanzania iwe chachu ya kushindania kombe hilo.
“Nina furaha kuwa hapa kwa ajili ya ziara ya kombe la Dunia kupitia Cocacola, ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania, kwa hiyo ni siku ya kipekee kwangu, kombe hili la Dunia ni sehemu ya mashindano ya FIFA Duniani, hapa anaangaliwa Mchezaji bora, kocha bora, kwa hiyo tuna kila aina ya ubora na ni mpira wa kipekee.
Ninapoangalia ziara hii nakumbuka furaha niliyokuwa nayo mwaka 2002 nikiwa na timu yangu wakati niliposhiriki michuano hii ya kombe la Dunia kule Japan na Korea Kusini, hususan kwenye nusu fainali na timu ya Uturuki nakumbuka ushindi, kwa hiyo furahieni kombe hili”,amesema Bw. Belleti