Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wadau wa kisiasa kukaa meza moja kwa ajili ya kupata maridhiano ili kujenga mazingira ya mwafaka kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema hayo leo Novemba 14, 2025 wakati akizindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, mabalozi, waheshimiwa wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, watendaji wa Serikali na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
"Sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano kupitia Tume ya Usuluhishi na Maelewano ili kwa
pamoja tujenge mazingira ya muafaka kwa maendeleo ya Taifa letu", amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa kama Taifa tunajifunza na kurekebisha makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia ili misingi yetu ya amani na utulivu iendelee kudumu.
Rais Samia amesema Tanzania ina uzoefu wa miongo mingi ya kuendesha demokrasia katika misingi ya amani, hivyo akiahidi kuendelea kuboresha ustawi wa taifa kulingana na mazingira na wakati.
"Ni jukumu letu sasa kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote. Naendelea kuwakaribisha vyama vya siasa, vyama vya Kijamii, Sekta binafsi na hata Jumuiya za Kimataifa ili kwa pamoja tuijenge Tanzania", amesema Rais Samia.