Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RAIS SAMIA: SERIKALI KUENDELEA KUZALISHA AJIRA NA KUIMARISHA MASLAHI YA WAFANYAKAZI
May 01, 2026
RAIS SAMIA: SERIKALI KUENDELEA KUZALISHA AJIRA NA KUIMARISHA MASLAHI YA WAFANYAKAZI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe, katika viwanja vya halmashauri ya mji wa Njombe ambapo alipokea maandamano ya wafanyakazi kutoka wizara mbalimbali pamoja na taasisi za umma na binafsi .
Na Baraka Messa – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imejikita katika kuimarisha uchumi wa nchi kwa lengo la kuongeza ajira zenye tija, kuboresha mazingira ya kazi na kuinua kipato cha wananchi, hususan vijana.

 

Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 1, 2026 wakati akizungumza na watumishi wa umma na sekta binafsi mkoani Njombe katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha ajira mpya zinatengenezwa pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi kadri uchumi wa nchi unavyoendelea kukua, sambamba na kuhakikisha ustawi wa wananchi unaimarika.

 

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali imefanikiwa kuwawezesha Watanzania 7,593 kupata ajira nje ya nchi, huku ikiendelea kusimamia haki, usalama na maslahi ya wafanyakazi hao wakiwa katika mataifa mbalimbali.

"Ajira 12,000 kwa vijana wa Kitanzania zimeshatengwa na zitatangazwa muda wowote, hatua hii inalenga kuongeza fursa za ajira na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini", amesema Rais Samia

Kuhusu vijana, Rais Samia amesema Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo kilimo, biashara na sekta nyingine zenye tija.

 

Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu katika uchumi na kujenga taifa lenye uzalishaji na maendeleo endelevu.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi