Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RAIS SAMIA, RUTO WAFUNGUA MILANGO YA BIASHARA HURU AFRIKA MASHARIKI
May 04, 2026
RAIS SAMIA, RUTO WAFUNGUA MILANGO YA BIASHARA HURU AFRIKA MASHARIKI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Na Baraka Messa – MAELEZO

Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto, amesema Kenya na Tanzania zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara, uchumi, ulinzi na usalama ili kuchochea maendeleo ya wananchi na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 4, 2026 baada ya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Ruto amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyokwamisha ukuaji wa biashara ya mipakani.

“Tunapaswa kuhakikisha bidhaa, huduma na watu wanatembea kwa uhuru ndani ya ukanda wetu ili kuchochea maendeleo ya pamoja,” amesema Rais Ruto.

Ameeleza kuwa mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha sekta muhimu zikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu na usafirishaji—nguzo kuu za ukuaji wa uchumi wa kikanda.

Rais Ruto amebainisha kuwa Kenya na Tanzania ni mhimili muhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kwamba ushirikiano wao utaimarisha soko la pamoja na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana.

Katika eneo la ulinzi na usalama, viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kukabiliana na changamoto za kiusalama na kuhakikisha utulivu unaohitajika kwa maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema nchi hizo zimepiga hatua muhimu kwa kusaini mikataba minane inayolenga kuimarisha mahusiano katika sekta za biashara, uchumi, nishati, usafirishaji na usalama, ikiwemo mapambano dhidi ya ugaidi na biashara ya dawa za kulevya.

Amefafanua kuwa miongoni mwa mikataba hiyo ni hati ya makubaliano ya ushirikiano katika uwekezaji na usimamizi wa reli kati ya Tanzania na Kenya, pamoja na makubaliano ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa.

Aidha, viongozi hao wamesaini mkataba wa usaidizi wa kisheria katika masuala ya jinai, pamoja na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya kilimo, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji na biashara ya mazao kati ya nchi hizo mbili.

Mikataba mingine inahusu utambuzi wa vyeti vya mabaharia, ushirikiano katika sekta ya maji, pamoja na kuoanisha viwango vya bidhaa kupitia taasisi za viwango za Zanzibar na Kenya ili kurahisisha biashara.

Pia, yamesainiwa makubaliano ya ushirikiano kati ya vyuo vya utumishi wa umma vya Tanzania na Kenya kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma serikalini.

Rais Samia amesisitiza kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo utafungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza ajira na kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Kenya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor