Na Shamimu Nyaki
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika kitaifa Julai 07, 2022 jijini Dar es Salaam
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 29, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla amesema kuwa, analishukuru Shirika la UNESCO nchini kwa kuendelea kuipa heshima lugha ya Kiswahili kwa kuadhimisha siku hiyo maalum kila Julai 7 ya kila mwaka.
"Maadhimisho haya kwa mwaka huu ni ya kipekee sana, tunatarajia kupata wageni wengi mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi, akiwemo Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chisano, Rais Mstaafu wa Namibia, Mhe. Sam Nujoma, hii ni heshima kubwa kwa mkoa wetu", alisema Mhe. Makalla.
Ameongeza kwa kueleza kuwa, maadhimsho hayo yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kongamano kuhusu mchango wa lugha ya Kiswahili katika Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika, litakalofanyika Julai 06, 2022 ambapo Balozi Mstaafu, Mhe. Ame Mpungwe ataongoza mada mbalimbali.
Maadhimisho hayo yatatanguliwa na Tamasha la Utamaduni la Kwanza Kitaifa ambalo litafanyika katika Uwanja wa Uhuru kuanzia Julai 01 hadi 03, 2022.