Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Mgeni Rasmi katika Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro
Jan 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi, WUSM- Moshi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro ambalo litafanyika Januari 22, 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika kilichopo Manispaa ya Moshi.

Taarifa ya Tamasha hilo imetolewa na Umoja wa Machifu wa mkoa huo chini ya Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro  Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu katika katika kikao cha Machifu wa mkoa huo kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi.

“Ni heshima mkoa wetu kuwa wa kwanza kutekeleza agizo la Chifu Mkuu, Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambalo alilitoa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba 2021 katika Tamasha la Utamaduni ambalo aliagiza mikoa yote nchini kuendesha matamasha ya utamaduni kwa lengo la kuelimisha jamii na kuendeleza utamaduni wetu” amesema Chifu Mareale. 

Akizungumzia Tamasha hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Temu amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeitikia agizo la Rais Mhe. Samia Suluhu ambapo alitoa maelekezo kwa mikoa yote nchini kufanya matamasha ya kiutamaduni katika maeneo yao.

“Tumeanza safari kubwa ya kuimarisha utamaduni wa Mkoa wa Kilimanjaro, Matamasha haya yatainua na kuibua hazina kubwa ya kiutamaduni miongoni mwa jamii iliyopo nchi nzima itakayotumika kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na yataleta” amesema Dkt. Temu.

Ili kulifanya tamasha hilo kuwa la jamii nzima, Dkt. Temu amesema kuwa vijana wahamasishwe kushiriki hatua itakayowasaidia kujifunza na kuonja uthamani wa utamaduni kama anavyoothamini Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaonesha kwa vitendo kwa kushiriki matamasha ya utamaduni nchini kudhihirisha kuwa utamaduni ni utajiri ambao unaweza kuwasaidia watu wote kuanzia vijana hadi wazee kama chanzo cha ajira kupitia utalii wa kiutamaduni katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Temu amesema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997, wananchi wana wajibu wa kuendeleza utamaduni na Serikali ikiwa na wajibu wa kusimamia mila na desturi na kuongeza kuwa tamasha la Kilimanjaro linatarajiwa kuwa na vionjo ambavyo vitakuwa na mvuto kwa watanzania kwa kuonesha vyakula vya asili vya kutosha, mavazi ya asili, ngoma za asili pamoja na historia ya makabila ya Wachaga, wapare, wamasai na wagwemo na kuwa tamasha la mfano ambalo litatoa hamasa kwa mikoa mingine kuandaa matamasha ya kiutamaduni katika mikoa yao.

Tamasha la Kilimanjaro ni utekelezaji wa Sera ya Utamaduni ambayo imetoa mwelekeo wa maendeleo ya utamaduni kwa kuainisha jinsi shughuli za utamaduni zitakavyoendeshwa na kusimamiwa pamoja na kuweka wazi majukumu ya Serikali, wananchi kwa makundi au mmoja mmoja na sekta binafsi ili kufanikisha lengo la kuhifadhi na kuuenzi utamaduni wetu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi