Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 19 Novemba, 2025 atapokea tuzo kutoka Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF) ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kandanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, atapokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Mji wa Rabat nchini Morocco.

Pamoja na Bw. Msigwa, hafla hiyo ya utoaji wa tuzo inahudhuriwa na Rais wa TFF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Bw. Wallace Karia na Mwenyekiti wa Vilabu Barani Afrika na Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said.
Tuzo hiyo inatolewa kwa Rais Samia kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha uongozi wake ya ujenzi wa miundombinu ya michezo vikiwemo viwanja vikubwa, kuwa wenyeji wa mashindano ya CHAN na maandalizi ya AFCON 2027 pamoja mafanikio makubwa ya Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
Mafanikio hayo ni pamoja na kupanda kwa ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania ambayo sasa ni ya 5 kwa ubora Bara Afrika, kuboresha soka la wanawake na kukuza soka kwa vijana.