Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Azindua Tume Huru Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29
Nov 20, 2025
Rais Samia Azindua Tume Huru Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mohamed Chande Othman katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo, Ikulu Chamwino, tarehe 20 Novemba, 2025.
Na Naishooki Makeseni - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Tume Huru ya uchunguzi wa matukio ya uchaguzi mkuu wa 2025, ikiwa ni hatua muhimu ya Serikali kuchunguza kwa kina matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akizindua tume hiyo leo Novemba 20, 2025 Ikulu, Chamwino Dodoma, Rais Samia amesema amefanya hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 2023, Sura ya 32 ambayo inampa mamlaka Rais kuunda Tume za kuchunguza masuala mbalimbali ya kitaifa.

Amesema tume hiyo itakuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, akiwashukuru wajumbe kwa kukubali uteuzi akieleza kuwa ana imani na tume hiyo kutokana na sifa na ubobevu wa wajumbe watakaofanya kazi ya uchunguzi wa matukio yaliyotokea.

Rais Samia amebainisha kuwa pamoja na mambo mengine tume hiyo itachunguza kwa kina sababu na kiini cha vurugu zilizotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu, madai na haki walizokuwa wanadai vijana ambazo ziliwafanya waingie barabarani.

Aidha, amesema mapendekezo ya tume hiyo yataweka msingi kuelekea uundwaji wa tume ya maridhiano, aliyoahidi kuiunda katika siku 100 za mwanzo wa muhula wa pili wa uongozi wake, itakayoshughulika na changamoto za kisiasa na kuweka misingi ya upatanisho wa kitaifa.

Hali kadhalika amesema tume hiyo itafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu, ikiendesha uchunguzi wa kina na baadaye kuwasilisha ripoti yake inayotarajiwa kuongoza hatua za Serikali katika kurejesha na kuimarisha amani, haki na maridhiano ya kitaifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi