Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Azindua Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe
Mar 09, 2025
Rais Samia Azindua Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria ufunguzi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe mara baada ya kuhutubia wananchi wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro tarehe 09 Machi, 2025.
Na Mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe utakaowahakikishia  wananchi wa miji ya Same, Mwanga na vijiji 38 vya wilaya za Same, Mwanga na Korogwe  huduma ya uhakika ya majisafi na salama.

Dkt. Samia  amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za kijamii hususan huduma ya majisafi, na kuongeza kuwa kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya mradi huo, kumeongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni  3.7 kwa siku hadi lita milioni 51.6  kwa siku, hatua inayotoa ahueni kubwa kwa wakazi wa wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.

“Mradi huu ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Same na Mwanga walioungojea kwa muda mrefu. Kupitia mradi huu, tatizo la upatikanaji wa maji sasa litakuwa historia,” Mhe. Rais Dkt.  Samia amesema.

Kwa upande mwingine,  ameeleza amefurahishwa na kukamilika na kuuzindua mradi huo aliouwekea Jiwe la Msingi tarehe tarehe 12 Novemba, 2018 akiwa Makamu wa Rais, akiishukuru Wizara ya Maji kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo na hatimaye kuukamilisha baada ya takribani miaka 20.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameagiza ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vya maji, ili huduma ya maji iwe toshelevu na endelevu. Amewataka wananchi walipe ankara za maji kwa wakati ili Mamlaka ya Maji ya Same-Mwanga iweze kujiendesha na kutoa huduma ya uhakika ya maji.

Amewashukuru washirika wa maendeleo wakiwemo Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa OPEC (OFID), Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait, na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD) kwa kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Wizara ya Maji na watumishi wote watafia katika uwanda wa kazi kwa kuhakikisha wanatimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, CCM (2020-2025), ambapo amesema mpaka sasa huduma ya maji vijijini imefika asilimia 83 kati ya 85 na mijini 91 kati ya 95 kama Ilani hiyo inavyoelekeza kufikia Disemba, 2025.

Pia, Mhe. Jumaa Aweso amepiga marufuku huduma ya maji kukatwa siku za Siku Kuu na mwisho wa juma  ili wananchi wafurahie huduma ya majisafi na salama ambayo wameisubiri kwa muda mrefu.

Mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe umegharimu jumla ya shilingi bilioni 406.07, ambapo shilingi bilioni 244.10 ni mkopo, na Serikali ya Tanzania imetoa shilingi bilioni 161.97.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi