Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Samia Suluhu Hassan leo Juni 19, 2022 amezindua Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake yenye kauli mbiu inayosema “lea mwana tung’are”.
Kabla ya kuzindua taasisi hiyo, Mhe. Rais Samia ameupongeza uongozi wa MIF kwa mkakati kabambe wa taasisi hiyo wa kuleta chachu ya kuunganisha Serikali na MIF na taasisi nyingine katika kumkomboa mtoto wa kike kielimu huku akielekeza Serikali inavyofanya maboresho izingatie masuala ya mitaala, ukaguzi wa elimu, utungaji wa mitihani na sifa za walimu.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kuunga mkono jitihada zinazofanywa na MIF huku akisisitiza kuwa suala la kuwakomboa Watoto wa kike ni suala la kila mtu. “Hili ni jukumu letu sote, tunatakiwa wote tushirikiane.” Ameongeza Mhe. Rais
Amezielekeza Wizara zinahusika na elimu kwa pande zote mbili za muungano kuhakikisha zinashirikiana ili kuhakikisha kuwa watoto wote wakiume na wakike wanatimiza ndoto zao kwa faida ya taifa zima.Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar amemshukuru Rais kwa kuja kuzindua taasisi hiyo huku akielezea kuwa kwa kuja kuzindua amewapa heshima kubwa wadau wote wa elimu nchini.
Amesema MIF inatambua kuwa kumekuwa na changamoto katika jamii inayowazunguka lakini wao wameamua kujikita katika elimu hususan kubadili mtazamo na fikra ya kuwa mtoto wa kike hana uwezo na badala yake ni kumkomboa ili hatimaye ayaishi malengo na ndoto za maisha yake huku akiiomba jamii iwaunge mkono.
Amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea kuchangia ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kutimiza ndoto zao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa MIF, Fatuma Mwasa ameyaelezea malengo makubwa ya taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kusaidia jamii huru iliyo na maendeleo isiyosumbuliwa na ujinga, umasikini na maradhi kwa kumwinua mtoto wa kike kielimu, kuwawezesha vijana kiuchumi, kuongeza uelewa katika afya ya akili na kushughulika na afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto.
Ameitaja baadhi ya mipango inayofanywa na MIF kuwa ni pamoja na kujenga kituo cha cha kisasa cha mafunzo maalum kama vile ushonaji na umeme kinatakachogharimu takriban Shilingi bilioni 15 kwa ufadhili wa nchi za Falme za Kiarabu.
Pia, kuendelea kuongeza mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na kuwachukua wanafunzi ambao hawajafanikiwa kwenye masomo na kuwa vhyuo vya ufundi ambapo amesisitiza kuwa wamekuwa wakifanya vizuri.
Ameongeza kuwa MIF inafundisha kilimo cha mbogamboga lengo ni kutaka kurudisha fedha mapema, pia inajenga vyoo katika shule, kutoa ufadhili wa kusomesha nje ya nchi wanafunzi wanaofaulu vizuri na kuwatafutia, masoko na mitaji.
Katika uzinduzi huo mawaziri anayesimamia elimu, Profesa Adolf Mkenda, anayesimamia Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa na anayesimamia Utumishi, Mhe. Jenista Mhagama wameungana na mawaziri kutoka SMZ kushiriki uzinduzi huo.