Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Mfumo wa Usafirishaji wa Dharura kwa Wajawazito na Watoto Wachanga (M-MAMA) unaosaidia kunusuru maisha ya wajawazito na watoto.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mfumo huo iliyofanyika leo jijini Dodoma, Rais Samia amesema mfumo huo umejaribiwa na kuonekana unafaa.
“Faraja niliyo nayo leo ni kuona mfumo huu tunaouzindua leo umekwishajaribiwa na kuonesha matokeo chanya katika kunusuru maisha ya mama mjawazito au mama mzazi na mtoto wake,” ameeleza Mkuu wa Nchi.
Sambamba na hilo, Mhe. Rais amefahamisha kwamba kukosekana kwa taarifa za haraka za usafiri ni moja ya sababu zinazochangia kupatikana kwa vifo vya wajawazito na watoto hivyo ameipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuja na mfumo wa M-MAMA ambao umeleta matunda kwenye Mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
“Sasa mpango huu unaendelea kupatikana kwenye mikoa 14 lakini wanavuka wanakwenda na Zanzibar,” amearifu Rais Samia.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema Serikali imekuwa ikitenga fedha kuwezesha utekelezaji wa miradi ya TEHAMA ili kuchochea uzalishaji na utoaji huduma wa sekta nyingine.
“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kutuongoza vyema katika kuvutia wawekezaji, kushirikisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuendeleza taifa letu,” ameeleza Mhe. Nnauye.
Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya TEHAMA ukiwamo usambazaji wa Mkongo wa Taifa na ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu unaofanywa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).