Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Awataka Vijana Kuchangamkia Fursa za TEHAMA
Apr 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, NewYork

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka watanzania hususan Vijana, kuchangamkia fursa za maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Rais ametoa wito huo Mjini NewYork nchini Marekani, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati alipozindua Mtandao wa NALA (NALA APP) utakaotumiwa na Watanzania waishio Marekani kutuma fedha nchini Tanzania kidijitali.

Alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NALA, Raia wa Tanzania, Bw. Benjamin Fernandes na Timu yake, kwa kubuni huduma hiyo ambayo itarahisisha utumaji wa fedha kutoka nchini humo kwenda Tanzania hatua ambayo itasisimua uchumi wa nchi na kuharakisha maendeleo ya wananchi watakaofaidika na huduma hiyo.

“Benjamin Fernandes na Timu yako ni miongoni mwa vijana wabunifu waliojikita katika masuala ya teknolojia ambao Serikali inawaunga mkono hususan wakati huu ambapo nchi inajenga uchumi wa kidijitali ambao matokeo yake yanatarajwa kuwa ni kukuza ajira, kuchangia Pato la Taifa na kukabiliana na changamoto zote za kiuchumi na kijamii”, Alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kujenga mkongo wa Taifa uliounganishwa na nchi nyingine za kiafrika zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya, Malawi, Uganda na Zambia na hivi karibuni nchi za DRC na Msumbiji zitaunganishwa.

Dkt. Nchemba alitoa wito kwa Wawekezaji kwenye sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuwekeza nchini Tanzania na kufaidi mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo nchi imeweka ili kuvutia mitaji na teknolojia.

Aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizoainishwa na uongozi wa Kampuni hiyo katika masuala ya upatikanaji wa leseni za kuendesha shughuli za TEHAMA ili kuwatia moyo vijana wabunifu wawekeze kwenye teknolojia zinazoweza kuchangia ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nimefahamishwa kwamba Marekani imewekeza karibu Dola bilioni 1.5 katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Barani Afrika, ninatamani kuona kuwa Tanzania inakuwa ni moja ya nchi zitakazonufaika na uwekezaji huo”, Alisisitiza Dkt. Nchemba katika Hotuba yake akimwakilisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw. Benjamin Fernandes alisema kuwahuduma hiyo iliyozinduliwa nchini Marekani, inafanyakazi katika nchini nyingine 9 duniani na aliibuni kwa ajili ya kusaidia utumaji wa fedha kwa nchi za Afrika. 

Aidha, Bw. Fernandes aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza masharti ya leseni ya biashara ya mitandao ili kuwawezesha vijana wengi wabunifu wa TEHAMA kuwekeza nguvu zao kwa kuwa itaongeza ajira na kukuza uchumi wao.

Alifafanua kuwa hivi sasa mtu anayetaka kutoa huduma ya kibunifu analazimika kulipia leseni Benki Kuu ya Tanzania hata bila kuanza kufanya kazi hatua ambayo alisema inawakwaza vijana wengi kutimiza ndoto zao za kujiajiri na kuwaajiri watu wengine.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi