Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya aliowaapisha leo Novemba 18, 2025 wawajibike kwa wananchi ili maendeleo yaweze kupatikana kwa haraka.
Rais Samia amesema hayo kupitia hotuba aliyoitoa mara baada ya uapisho wa Mawaziri 27, na Naibu Mawaziri 29 ili kuanza utekelezaji wa majukumu ya muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya sita.
Amesema kazi kubwa ambayo iliyo mbele yao ni kuwajibika kwa wananchi na kwa Taifa la Tanzania kwa kuwa Serikali imewaahidi mambo mengi wananchi ambayo yanahitaji kasi kubwa ya utekelezaji na usimamizi
"Majukumu tuliyopeana leo ni dhamana ya kazi. Tumebeba wajibu wa kwenda kuwatumikia wananchi yakiambatana na kauli mbiu yetu ya kazi na utu tunasonga mbele" Ameeleza Rais Samia na kuongeza kuwa miaka mitano sio mingi kwa kuzingatia wingi wa mambo yayoahidiwa kwa wananchi hivyo mawaziri walioapishwa wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii.
Mawaziri wapya walioapishwa wanachukua nafasi katika kipindi ambacho Serikali imejipanga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na miundombinu, elimu, afya, usafirishaji na huduma mbalimbali za kijamii.