Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Awataka EALS Kutenda Haki
Nov 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Daudi Manongi, ARUSHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wanasheria kusimamia haki katika kesi mbalimbali wanazozisimamia.

Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2022 wakati akifungua mkutano wa 27 wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) uliofanyika katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

“Msipofanya haki, mnapomtia mtu hatiani
kwa rushwa ambaye hana hatia na mwenye hatia mkamuachia anatembea huru yule mwenye hatia anakwenda kuendeleza ubabe na kuvunja sheria akijua pesa yake itambeba na yule ambaye hana pesa anaishia jela”, amesema Rais Samia.

Aidha, ametoa rai kwa Jumuiya hiyo kuendelea kushirikiana bega kwa bega na vyama vingine vya Wanasheria wa kitaifa ili kukuza utoaji wa haki na kusimamia uzingatiaji wa sheria katika Jumuiya yetu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda ametoa rai kwa wanasheria nchini kujiunga na Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki kwa sababu ni chombo muhimu kitakachowatangaza ndani na nje ya nchi.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Bernard Oundo amesema Mkutano huo utawasaidia kujadili faida za umoja na utofauti wao kama Wanasheria lakini namna gani wanaweza wakajiweka kwa ajili ya faida zaidi katika kufanya kazi za kisheria kiulimwengu.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Prof. Edward Hoseah amesema wao wako tayari kushirikiana na Serikali zote za Afrika Mashariki ili kuona kwamba utawala wa sheria na misingi ya demokrasia inazingatiwa.

Mkutano huo wa 27 wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 23- 26 Novemba, 2022 na unakutanisha wanasheria zaidi ya 600 kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi