Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa habari kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhabarisha umma hasa kuhusu habari za maendeleo ya nchi.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Uandishi wa Habari ‘Samia Kalamu Awards’ zilizofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini Mei 5, 2025, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki Dar es Salaam.
Sambamba na hilo, amesisitiza uzalendo na utu kwa taifa kupitia taarifa au habari mbalimbali zinazoandikwa.
“Uhuru wa vyombo vya habari unakua na unaendelea kukua na takwimu zinasema zenyewe, Tanzania uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa, lakini kuwa na uhuru wa habari si kukosa uzalendo kwa nchi yako, tuipende nchi yetu” amesema Rais Samia.
Vile vile, Mhe. Rais Samia amehimiza kujipanga vema katika katika kipindi hiki ambapo nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, kwamba wanahabari wanapaswa kuwa chanya katika utoaji wa habari zao ili kulinda amani ya nchi.
“Tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu baadae mwaka huu, waandishi tumieni vema taaluma yenu kuiunganisha nchi ili tuendelee kuwa wamoja, kalamu zenu zilinde na kuitetea nchi yetu sawa sawa na jeshi linavyolinda, tukizitumia vizuri tutakuwa salama, zikitumika vibaya hatutakuwa salama” amesisitiza Mhe. Rais Samia.
Kwa upande wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba John Aisan Mwaluko Kabudi, amesema kwamba zawadi hizo zilizotolewa kwa waandishi wa habari, zitakuwa ni kichocheo kwao kuendelea kujikita katika maeneo ambayo wamepewa tuzo na kufanya vizuri zaidi.
“Tumeamua kuhamasisha tena uandishi wa habari za maendeleo, lengo likiwa ni kuibua masuala ya maendeleo yanayoendelea ndani ya nchi ili dunia nzima iyafahamu. Sasa tunatoka katika uandishi wa habari wa jumla na kuhamia kwenye uandishi ambao mwandishi ametabahari katika eneo hilo” amesema Mhe. Waziri Kabudi.
Waandaaji wa tuzo hizo za ‘Samia Kalamu Awards’ ambao ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), nao walitanabahisha umuhimu wa jambo hilo kwa wanahabari na jamii pia.
“Naamini tuzo hizi zitaleta chachu na mabadiliko makubwa kwenye tasnia ya habari kwa kuongeza thamani kwenye kazi zao na kuwa mfano bora kwa waandishi wengine wanaowazunguka pia zitakuwa ni kielelezo cha dhamira thabiti ya Serikali ya kuinua hadhi na heshima ya tasnia ya habari nchini”, alieleza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Joyce Shebe amesema tuzo hizo ni mahsusi kwa aandishi wa habari za maendeleo ambapo lengo kuu ni kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo jumuishi, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira chanya ya Tanzania.
“Jumla ya wanahabari 2,054 walishiriki mafunzo hayo lengo likiwa ni kukumbushana wajibu wa msingi wa kuwahabarisha Watanzania kupitia habari zenye tija zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina” ameongeza Bi. Shebe.