Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, katika mkoa wa Tanga imezidi kuunemesha mkoa huo kiuchumi baada kuahidi kuwajengea kiwanda kikubwa cha sukari ya viwandani.
Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo Februari 26, 2025 wakati akihutubia wananchi wilayani Pangani mkoani Tanga, ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake katika mkoa huo.
Amesema kujengwa kiwanda cha sukari ya viwandani kutachochea ukuajia wa uchumi na kuufungua mkoa wa Tanga kiuchumi na kuongeza kuwa mbali na kufungua kiwanda cha sukari, Serikali itaanzaisha shamba kubwa la miwa katika wilaya ya Pangani na hivyo kuzidi kukuza fursa za kiuchumi na kukuza ajira.
Aidha, Rais Samia amesema kiwanda hicho kitasaidia kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza sukari ya viwandani nje ya nchi.
Rais Samia ametaja miradi mingine katika mkoa huo ni pamoja na soko la kimataifa la samaki katika wilaya ya Pangani ambalo litasaidia kuongeza ajira na pia ujenzi wa barabara ya Bagamoyo - Pangani hadi Tanga utaufungua mkoa huo na ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara yake katika mkoa wa Tanga imeingia siku ya nne ambapo ametembelea kukagua, kuzindua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Pangani.