Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza baraza jipya la mawaziri lenye jumla ya Wizara 27 ikiwemo wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais.
Akitangaza baraza hilo leo Novemba 17, 2025 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia amemteua Mhe. Joel Arthur Nanauka Mbunge wa Mtwara Mjini kuwa waziri wa Maendeleo ya Vijana akieleza kuwa wizara hiyo imeundwa kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika maamuzi na utatuzi wa kero zinazowakabili kama alivyoahidi wakati akifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 14, 2025 Jijini Dodoma
"Kama nilivyosema nilivyokuwa nahutubia Bunge kwamba tumeona umuhimu wa vijana kuwa na wizara kamili ambayo itasimama nao ambayo itakuwa chini ya Rais ", Amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameiboresha Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na kuwa Wizara ya Kazi, Ajira na mahusiano itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiongozwa na Mhe. Deus Sangu ambaye atakuwa na jukumu la kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ili kujenga mahusiano mazuri nchini.