Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuagiza mambo kadhaa ya kupewa kipaumbele yakiwemo ya ukuaji wa uchumi kufungamanishwa na sekta za uzalishaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara pamoja na uzinduzi wa mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu dira hiyo, rais amesema kilimo ni mfano wa sekta inayokua kwa asilimia 4, ambapo lengo la taifa ni kuhakikisha inakuza sekta hiyo.
"Kuna mambo tunapaswa kuyatazama wakati tunakamilisha utekelezaji wa dira ya sasa ya 2025, tunapoandaa dira mpya ya 2050, maeneo tunayopaswa kuyaangalia na kupewa kipaumbele katika dira mpya ni ukuaji wa uchumi kufungamanishwa na sekta za uzalishaji, kama sekta za kilimo na nyinginezo, ambapo sekta ya kilimo kwa sasa inakua kwa asilimia 4, lengo ni kuendelea kukuza sekta hiyo," amesema Rais samia.
Amesema Dira ya Maendeleo ya 2025 ilijengwa katika nguzo kuu nne ambazo ni kuboresha hali ya maisha ya watanzania, kuwepo kwa mazingira ya amani, utulivu na umoja, kujenga utawala bora na wa sheria na kujenga uchumi imara.
Amesema matarajio ya dira inayoandikwa sasa iweke lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji chakula barani Afrika na duniani.
Eneo lingine ambalo Rais samia amependekeza lifanyiwe maboresho ni kupata takwimu sahihi za uchumi kutoka sekta binafsi, kuongeza pato la wananchi, tathmini na ufuatiliaji pamoja na uratibu wa kufungamanisha vipaumbele kwa sekta zinazohusika na uzalishaji.
Eneo la tano ambalo rais amelitaja ni mchango wa mashirika ya umma katika kukuza uchumi wa nchi, na eneo la sita ni ushiriki wa sekta binafsi za ndani na nje ya nchi.
Rais ameyataja maeneo mengine mawili ya mwisho kuwa ni maadili ya taifa pamoja na kubaini viashiria hatarishi na kuviwekea udhibiti huku akitolea mfano majanga ya kimazingira, kiafya pamoja na uvunjifu wa amani kwenye baadhi ya nchi.