Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya walioapishwa wawekeze nguvu zaidi katika kutumia mapato ya ndani kutoka kwenye rasilimali zinazopatikana nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Novemba 18, 2025 wakati akiwaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma akiweka msisitizo kwa viongozi hao kuhakikisha wanatoa matokeo chanya kwa wananchi.
Amesema kutokana na changamoto za vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 huenda zikaipunguzia sifa Tanzania ya kupata mikopo kwa urahisi kama ilivyokua katika muhula uliopita akibainisha kuwa taifa linatakiwa kujipanga kutumia rasimali zake za ndani badala ya kusubiri misaada na mikopo kutoka kwa wafadhili, taasisi za fedha za nje na wadau wa maendeleo duniani.
"Tuna kazi ya kutafuta fedha humu ndani, kutumia rasilimali zetu za ndani alizotupa Mungu ili tupate fedha za kutekeleza miradi yetu. Muhula huu wa pili wa Awamu ya Sita tutaanza kufanya miradi yetu yote wenyewe hatutasubiri vyanzo vingine vya nje kama vile mikopo, kama ikija itatukuta tukiwa tunaendelea na kazi," amesisitiza Rais Samia.
Amewaasa Mawaziri na Naibu Mawaziri kutokuubeba Uwaziri kama fahari , bali wafanye kazi kwa maslahi ya Watanzania ili kuboresha maisha ya wananchi.