Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia kutoa kibali cha ajira mpya kwa watumishi wa umma 41,500 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutoa ajira kwa Watanzania.
Hatua hiyo imethibitishwa leo Januari 30, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya wizara yake katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa muhula wa pili wa Rais Samia.

Waziri Kikwete amesema ajira hizo zitahusisha kada mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, ualimu, kilimo, uvuvi, uhandisi, zimamoto na uokoaji, uhamiaji, magereza, Jeshi la Polisi pamoja na kada za utumishi wa umma.
Amesema utoaji wa ajira hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma, pamoja na kuchangia katika kutatua changamoto ya ajira kwa Watanzania.
kuhusu watumishi wanaoajiliwa kuomba maombi ya kubadilishiwa vituo vya kazi amesisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya vituo vya kazi kwa sasa kutokana na kazi hizo kutolewa kulingana na uhitaji.

"Nafasi zote zimetolewa kulingana na uhitaji wa kila eneo husika hivyo kubadili kituo cha kazi maana yake ni kupunguza idadi ya watumishi waliopangwa kwenye Halmashauri husika " amesema Kikwete .
Aidha Waziri Kikwete amewasihi vijana wenye sifa kuendelea kuomba nafasi mbalimbali kadri zitakavyoendelea kutangazwa na sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma ili waendelee kunufaika kupata nafas serikalini.