Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Arejea Nchini Kutokea Marekani
Sep 26, 2021
Na Jacquiline Mrisho

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 25 Septemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea New York nchini Marekani alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla, viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa, viongozi wa dini pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam, 

Wananchi hao wamesema wamejitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Rais Samia na kumpongeza kutokana na kuiwakilisha vyema Tanzania kupitia hotuba yake aliyoitoa tarehe 23 Septemba, 2021 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mhe. Rais Samia amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Watanzania wote kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kueleza kuwa hotuba yake ilijikita katika mambo makuu manne.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoukabili ulimwengu.

Mhe. Rais Samia katika hotuba yake pia ameeleza jinsi Tanzania inavyoungana na mataifa mengine kupambana na ugonjwa wa Virusi vya Korona, (UVIKO 19), juhudi za Serikali katika kukuza uchumi na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.

Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kuungana na kushirikiana kwa pamoja ili kuendelea kuijenga Tanzania madhubuti ambayo imejengwa kwa zaidi ya miaka 60.

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi