Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutoa elimu katika mazingira bora inayoendana na mazingira na soko la ajira.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 3, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi stadi.
"Serikali ilitenga shilingi bilioni 103 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 64 vya wilaya na kimoja ngazi ya mkoa", alieleza CPA Kasore
Akieleza mafanikio ya uwekezaji huo CPA Kasore amesema umewezesha kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga na kupanua vyuo vya ufundi stadi,kuhuisha mitaala,kubuni programu mahsusi za kuwezesha vijana, wanawake na makundi mbalimbali kupata ujuzi.
Aidha, CPA Kasore amesema jitihada za Serikali kujenga vyuo vipya na kukarabati vya zamani ikiwemo uwekaji wa vifaa vya kisasa ili mafunzo yatolewe kwa mifumo ya kisasa kwa ujumla kazi zote kwa miaka minne zimegharimu Serikali bilioni 233.7
Amesema VETA imehuisha mitaala 42 na kuanzisha mipya 20 katika sekta za TEHAMA, michezo, umeme, magari, mitambo, kilimo, ukarimu, usafirishaji,biashara, mavazi, madini na urembo.
Kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali,CPA Kasore amesema utawezesha ongezeko la udahili wa wanafunzi 89,700
" Kuhusu baadhi ya makundi yaliyonufaika na mafunzo ya VET amesema ni pamoja wajasiriamali 4,401 waliojengewa uwezo wa kuongeza tija kwenye shughuli zao na wanagenzi 5,175 waliotambuliwa na ujuzi wao kurasimishwa wakiwemo walioshiriki ujenzi wa reli ya SGR na Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).
Mwelekeo wa VETA baadae ni kutoa tunuku za kimataifa,kuimarisha ushirikiano na viwanda katika utoaji mafunzo,kushirikiana na mafundi mahiri katika kutoa mafunzo, kuimarisha ushirikiano na vyuo vya nje ya nchi.