Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, Maaskofu, Mapadri, Watawa, familia, ndugu, jamaa, marafiki, waumini wa Kanisa Katoliki na Watanzania wote kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Pengo, akieleza kuwa Taifa limepoteza kiongozi wa kiroho mwenye busara na mchango mkubwa katika kujenga maadili na mshikamano wa kitaifa aliyetoa huduma ya muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki na Taifa kwa ujumla.
“Katika kipindi chote cha utumishi wake, Kardinali Pengo alisimama imara katika kuhubiri amani, maadili na mshikamano wa kitaifa. Alikuwa sauti ya busara katika masuala ya kijamii na kimaadili, akihimiza amani, heshima na utu katika jamii yetu,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa mchango wa marehemu katika malezi ya kiroho na maendeleo ya jamii utaendelea kukumbukwa na kuenziwa daima na Watanzania wa rika zote.
Rais Samia ametoa pole kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference), Askofu Wolfgang Pisa, Maaskofu, Mapadri, Watawa, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na waumini wote wa Kanisa Katoliki pamoja na Watanzania kwa ujumla. “Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” ameongeza Rais Samia.