Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Ampa Tabasamu Mtoto Mwenye Tatizo la Moyo
Apr 14, 2026
Rais Samia Ampa Tabasamu Mtoto Mwenye Tatizo la Moyo
Picha kutoka maktaba: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Mtoto Selina Daudi anayekabiliwa na changamoto ya tundu kwenye moyo ameanza rasmi safari ya matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufuatia kupatiwa msaada wa kifedha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Selina anayeishi na mama yake Aisha Said katika eneo la Chanika jijini Dar es Salaam anatarajiwa kupata huduma za kibingwa zitakazomsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida kiafya.

Akizungumzia hatua hiyo leo Aprili 14, 2026 jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Peter Kisenge alisema msaada uliotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia umefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa mtoto huyo huku gharama za matibabu zikifikia zaidi ya shilingi milioni nane.

Mbali na msaada huo Dkt. Kisenge alieleza kuguswa na hali ya mtoto huyo na kuamua kujitolea kugharamia masomo yake yote huku akiahidi kulipia ada ya shule kupitia kipato chake binafsi.

Kwa upande wa huduma za kitabibu Daktari bingwa wa watoto wa JKCI, Sulende Kubhoja alibainisha kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yameongeza uwezo wa wataalamu kugundua mapema matatizo ya moyo kwa watoto na kutoa tiba stahiki kwa wakati.

Aliongeza kuwa kila siku taasisi hiyo hupokea watoto wengi wenye matatizo ya moyo ambapo wastani wa wagonjwa 50 wanaopekelewa kati yao takribani 20 huhitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Naye mama wa mtoto huyo Aisha Said alishukuru kwa msaada alioupata na kusema kuwa umempa faraja kubwa na moyo wa matumaini kwake na familia yake.

“Kwa kweli nina shukrani nyingi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia kwa msaada huu. Naamini mwanangu atapata matibabu na kupona na kuendelea na maisha kama watoto wengine ambao hawana matatizo ya moyo”, alisema Aisha.

Hatua hiyo inaendelea kuonesha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wananchi hususan wenye mahitaji ya matibabu ya kibingwa wanapata huduma muhimu kwa wakati.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi