Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ndani ya kipindi cha mwaka mmoja cha utawala wake, kutoa hati fungani ya shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kuulipa mfuko wa PSSF deni lilodumu kwa muda mrefu la shilingi trilioni 4.6 la michango kabla ya 1999 (pre-99).
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuonyesha nia ya kuufanya mfuko uwe stahimilivu na endelevu kwa ustawi wa wanachama kwa kulipa madeni. Wakati wa kuunganisha mifuko PSSF ilirithi madeni ya Serikali yaliyohakikiwa kutokana na PSSF kuwekeza kwenye miradi ya serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 731. Mpaka sasa serikali imeshalipa shilingi bilioni 500, ambapo shilingi bilioni 200 zimelipwa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita”, amefafanua Mhe. Ndalichako.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo Ijumaa, tarehe 11 Machi, 2022. jijini Arusha alipokuwa akizindua Bodi ya Wadhamini ya PSSSF iliyoteuliwa Desemba mwaka jana na kuitaka Bodi hiyo kuhakikisha PSSSF inawekeza kwenye miradi yenye tija ili Mfuko uendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, kwa kuwekeza kwenye viwanda vyenye uhakika wa kuongeza ajira na vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenyre Ulemavu, Prof. Jamal Adam Katundu ameitaka Bodi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili Bodi hiyo iweze kuisaidia PSSSF kufanya kazi kwa ufanisi ya kukusanya michango, kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama, kulipa mafao na kuwekeza kwenye miradi yenye tija.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba amebainisha kuwa thamani ya Mfuko imekuwa hadi kufikia shilingi trilioni 8.24 ukilinganisha na shilingi trilioni 7. 04 zilizokuwepo wakati Mfuko unaanza, Gharama za uendeshaji wa Mfuko zimepungua kutoka TZS. 128.93 bilioni mwaka 2018 hadi TZS. 68.83 bilioni mwaka 2020/21 sawa na kushuka kwa asilimia 46.61.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ,Mhandisi Musa Iyombe amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa maelekezo watayatekeleza kikamilifu na Bodi hiyo kuwa itafanya kazi yake ya kumshauri kwa uaminifu , uadilifu na weledi.
Bodi ya wadhamini iliyozinduliwa inajumuisha; Mhandisi Musa Iyombe ambaye ni Mwenyekiti, wajumbe ni; Dkt. Aggrey K. Mlimuka, Bi. Suzan B. Kabogo, CPA Stella E. Katende, Bw. Victor F. Kategere, Bi. Mazoea Mwera, Bw. Thomas C. Manjati, Bw. Said A. Nzori na Bw. Rashid M. Mtima.