Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwathamini wawekezaji kwa kuridhia kupunguzwa na kufutwa baadhi ya tozo zilizokuwa zikitozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) zenye thamani ya shilingi bilioni 35.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo leo Agosti 18, 2023 jijini Dodoma kwenye kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya OSHA.
Alisema hatua hiyo ilitokana na ombi la wafanyabiashara kupitia Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) ili kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji nchini.
Katambi alisema masuala ya usalama na afya mahali pa kazi yataendelea kupewa uzito na serikali ili kuhakikisha nguvu kazi iliyopo inakuwa salama.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatuma Toufiq alipongeza serikali kwa kuendelea kufanyia kazi maoni ya kamati ya kuimarisha masuala ya usalama mahali pa kazi kwa kuipatia OSHA vitendea kazi ili itekeleze majuku yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema tozo ya upimaji umeme katika vituo vya mafuta hasa maeneo ya vijijini imepunguzwa kutoka shilingi 650,000 hadi shilingi 150,000 ili kuvutia wawekezaji na kuondokana na mafuta kuuzwa kwenye chupa.
Alisema kumekuwa na matokeo chanya ambapo OSHA imevifikia vituo 2,708 ikilinganishwa na kabla ya kupunguzwa tozo vilifikiwa vituo 1,153.
Kadhalika, alisema kutokana na Tanzania kutekeleza kwa kiwango kikubwa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, imekuwa mfano kwa mataifa mengine kuja kujifunza.