Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Aipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Jan 30, 2024
Rais Samia Aipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akielezea kuhusu samaki wa aina mbalimbali wanaopatikana katika Ziwa Victoria mara baada ya uzinduzi wa boti za kisasa pamoja na vizimba vya kufugia samaki Jijini Mwanza tarehe 30 Januari, 2024.
Na Edward Kondela

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Uvuvi, hivyo imeamua kutoa kipaumbele katika kukuza sekta hiyo kwa kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amebainisha hayo leo (30/01/2024) jijini Mwanza, wakati wa kukabidhi boti 160 na vizimba 222 kwa wanufaika kwenye Kanda ya Ziwa Victoria na kuitaka wizara kubuni mbinu zaidi za kuhakikisha inawezesha wanufaika wengi zaidi kupitia rasilimali za uvuvi.

Ameongeza kuwa, kwa sasa wizara imekuwa ikifanya mambo mengi makubwa na yenye kuleta tija kwa wananchi ambapo katika Sekta ya Uvuvi wananchi wengi wamekuwa wakitegemea sekta hiyo kwa ajili ya kujipatia kipato.

Pia amewataka wanufaika wa boti za uvuvi na vizimba kuhakikisha wanatumia vyema zana hizo na kuzitunza pamoja na kuondokana na migogoro yoyote ambayo inaweza kujitokeza kwenye vikundi vyao kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha mradi huo unaenda maeneo mengi zaidi hapa nchini.

Aidha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024 wizara hiyo ilipatiwa fedha shilingi bilioni 60 kila mwaka kwa miaka miwili mfululizo ili kukuza Sekta ya Uvuvi.

Pia Mhe. Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, nia ya wizara ni kusambaza boti za uvuvi zisizopungua 500 kote nchini ili kuwezesha wanufaika wengi zaidi kwa kuwa sekta hiyo inatoa ajira kwa watu milioni 4.5.  

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, amesema wizara itahakikisha inaendeleza maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inazidi kutoa ajira zaidi kupitia zana mbalimbali zikiwemo boti na vizimba ambavyo amevigawa leo kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji kupitia mkopo usio na riba.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Amos Makala amesema hafla ya kukabidihi boti 55 na vizimba 222 kwa mkoa huo, utakuza uvuvi endelevu kwa kuwa amekutana na wadau wa uvuvi ambapo tafiti zinaonesha samaki ndani ya Ziwa Victoria wamepungua kwa asilimia 30 na kuathiri baadhi ya viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, kutokana na kukithiri kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu na kwamba mkoa tayari umeweka mikakati mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo.

Nao baadhi ya wanufaika wa boti na vizimba wameshukuru kwa kupatiwa zana hizo pamoja na vifaranga  vya samaki na chakula cha samaki, wameiomba serikali kuwahakikishia mbegu bora za vifaranga vya samaki pamoja na chakula ili waweze kufuga kibiashara na kukuza kipato chao na hatimaye kuweza kurejesha mikopo.

Pia wamesema wamefurahia kupatiwa boti za kisasa na zenye injini za kupachika ambazo ni imara hivyo watahakikisha wanatumia vyema boti hizo ili waweze kurejesha mikopo na kuweza kukopa kwa awamu nyingine.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi