Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Ahudhuria Dhifa ya Kitaifa Jijini Bujumbura
Jul 18, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 16 Julai, 2021 amehudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Rais Evariste Ndayishimiye Ikulu Jijini Bujumbura.

Akizungumza wakati wa Dhifa hiyo Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Rais Ndayishimiye kwa kazi kubwa anayoifanya tangu ashike madaraka ya kuiongoza nchi hiyo.

Mhe. Rais Samia amesema Mhe. Rais Ndayishimiye katika kipindi kifupi cha utawala wake ameongoza mapambano dhidi ya rushwa, ameanzisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii, ameimarisha amani na usalama na kuimarisha uhusiano na nchi mbalimbali pamoja na taasisi za kimataifa.

Kufuatia jitihada hizo, Mhe. Rais Samia amezitaka nchi na taasisi za kimataifa ambazo bado hazijaondoa vikwazo kwa Burundi kufanya hivyo ili nchi hiyo iweze kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na Burundi ambapo viongozi hao wamekubaliana kuondoa vikwazo ili kuongeza biashara na uwekezaji katika mataifa yao.

Katika kukuza biashara na uwekezaji, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Huduma za Pamoja kwenye mpaka katika eneo la Manyovu na Mugina. Pia wamekubaliana kushirikiana kwenye ujenzi wa barabara, ikiwemo Barabara ya Nyakanazi – Kasulu – Manyovu /Rumoge – Gitaza pamoja na Reli ya Uvinza – Msongati – Gitega.

Kwa upande wake Mhe. Rais Ndayishimiye amempa pole Mhe. Rais Samia na Watanzania kwa ujumla kwa hasara kubwa waliyoipata kufuatia kuungua kwa Soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema hasara hiyo si kwa Wafanyabiashara wa Tanzania pekee bali hata Warundi kwani Soko hilo si kwamba linahudumia Tanzania pekee bali nchi nyingi za Afrika Mashariki ikiwemo Burundi.

Mhe. Rais Ndayishimiye amemshukuru Rais Samia kwa kufanya ziara nchini Burundi na kusema kuwa ziara hiyo imedhihirisha uhusiano na ushirikiano wa kweli uliopo kati ya Tanzania na Burundi.

Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi