Na Grace Semfuko MAELEZO- Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu ya royal tour utakaofanyika Jumamosi Mei 7 mwaka huu Visiwani humo.
Filamu hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa New York na Los Angeles- California nchini Marekani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa nchini Tanzania ilizinduliwa Aprili 28 Jijini Arusha ambapo sasa inasubiriwa kwa hamu kubwa kwa wakazi wa Zanzibar.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Zanzibar leo Ijumaa Mei 6, 2022, Mwenyekiti wa Taifa wa Kamati ya filamu ya royal tour, Dkt. Hassan Abbasi amesema uzinduzi wa filamu hiyo Visiwani Zanzibar una tija kubwa kutokana na historia yake katika sekta ya Utalii pamoja na kutoa heshima kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mzaliwa wa visiwani humo.
Amesema kwa kipindi kifupi filamu hiyo inatarajiwa kutazamwa na watu zaidi ya bilioni Moja duniani kote ikiwa ni kufikia lengo la kuitangaza Tanzania Katika Sekta ya utalii na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa Nchini.
Dkt. Abbasi amesema kuwa filamu hiyo imeshaanza kuleta faida kubwa tangu alipozinduliwa nchini Marekani na hapa Tanzania na kwamba baada ya kuzinduliwa Mei 7 kuzinduliwa Zanzibar, itafuatia Jijini Dar es Salaam Mei 8 mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere -JNICC.
Aidha, amefafanua kuwa filamu ya The Royal Tour imekuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu kuzinduliwa ambapo matajiri na wafanyabiashara wakubwa Marekani wameonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania Katika Sekta mbalimbali ikiwemo viwanda na maeneo ya utalii ili kuvutia zaidi watalii kote ulimwenguni.
"Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuitangaza Tanzania akishirikiana kwa ukaribu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mwinyi Katika kuifanyia hii filamu kuwa ya kipekee na kuvutia watu wengi ulimwenguni na hapa lengo la kuitangaza Tanzania duniani limefanikiwa kwa kuonesha mfano kwa viongozi hawa wawili kushiri kwa vitendo ndani ya filamu hii" amesema Dkt. Abbasi.
Aidha, amesema kuwa lengo la kushirikiana na waandaji wa kimataifa kufanya filamu hii ilikuwa ni kutaka kuwafikia watu wengi zaidi duniani na wazoefu katika kazi hizi na kueleza kuwa haki miliki za filamu hii zipo vizuri na Tanzania itanufaika zaidi Kutikana na kuzalisha filamu hiyo ambayo Wadau mbalimbali ndio wamechangia kugaharamia maandalizi ya filamu hii bila kutumia pesa kutoka Serikalini.
Watanzania wanatarajia kuona uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour tarehe 8 Mei ambapo vituo vyote vya televisheni nchini vitapewa hati miliki ya kurusha filamu hiyo ili kuwawezesha watanzania kwa wingi kujionea namna utalii wa Tanzania ulivyotangazwa na viongozi Wakuu huku juhudi za kuirusha vyombo vingine ulimwenguni zikiendele huku kukiwa tayari Kuna makubaliano ya kuirusha filamu hiyo chaneli ya Apple na Amazoni ambazo zina watazamaji wengi ulimwenguni.