Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam alipokuwa akikagua jengo hilo jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2021.
Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya reli kwa kujenga reli mpya ya kisasa ili kuliongezea Shirika la Reli ufanisi katika kubeba mizigo.
“Serikali ya Tanzania inawekeza katika uboreshaji miundombinu ya zamani na kujenga miundombinu mipya ya kisasa ili kuendana na uchumi mzuri kwa nchi za Afrika Mashariki", ameongeza Waziri Makame Mbarawa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR ameeleza kuwa kwa sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza yenye urefu wa Kilometa 1219 kwa njia kuu.
Kadogosa ameongeza kuwa, ujenzi wa reli ya kisasa utasaidia kukuza uchumi na utaunganisha kibiashara nchi za Afrika Mashariki kupitia bandari na ziwa Victoria kwa kuokoa muda wa safari na gharama za usafirishaji hadi 40%.
Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (kulia) akipata maelezo kuhusu eneo ambalo litatumika na abiria wakati wa kupanda na kushuka katika treni za kisasa za SGR katika Stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2021.
“Usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni kwa kutumia treni za kisasa utarahisisha zaidi na kuokoa muda, safari moja ya treni itakua na uwezo wa kusafirisha Tani 10,000", amesema Kadogosa.
Aidha, Kadogosa amesema kuwa TRC imeweza kurejesha huduma ya usafirishaji wa shehena ya mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Kampala nchini Uganda kupitia reli, pia TRC inaendelea na jitihada za kuboresha huduma za usafiri wa reli kati ya Tanzania na Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Reli Uganda kwa lengo la kuzifaidhisha nchi ya Uganda na Tanzania kupitia Bandari.
“Hivi karibuni miezi miwili iliyopita tumeanza biashara ya mafuta, yanatoka bandari ya Dar es Salaam yanapita ziwa Victoria na kufika Port Bell nchini Uganda, na mpaka sasa tumeshapeleka matenki 72 ambayo ni sawa na lita milioni 3,240,000, ni huduma ambayo ilipotea na tumerudisha”
Kadogosa amesema kuwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro umefika zaidi ya 95%, Morogoro – Makutupora ambao umefika 75% pamoja na Isaka - Mwanza ambao umefika 3.87%, huku vipande vya Makutupora – Tabora na Tabora – Isaka vikiwa kwenye maandalizi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.