Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia.
Akitoa taarifa ya kifo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kifo cha Rais Mstaafu, Hayati Mwinyi kimetokea leo Februari 29, 2024 majira ya saa 11:30 jioni jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena.
"Kwa niaba ta Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu," ameeleza Rais Samia kwa masikitiko makubwa.
Aidha, Rais Samia amearifu kuwa mwili wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi utazikwa Machi 2, 2024 huko Unguja, Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Samia ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kama ishara ya msiba wa kitaifa.
Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi atakumbukwa kwa jina la "Mzee Ruksa" kutokana na umahiri wake wa kutekeleza maono ya Mwalimu Julius Nyerere ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa la kidemokrasia linaloheshimu uhuru na haki za binadamu huku likiongozwa kwa misingi ya kijamaa.