Na Fatma Salum
Usimamizi mzuri wa fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini chini ya uongozi imara wa Rais John Pombe Magufuli, umeiwezesha Tanzania kuendelea kupata wafadhili wengi kutoka nchi za nje na mashirika ya kimataifa.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ni miongoni mwa taasisi inayosaidia Tanzania katika juhudi za kukuza na kuimarisha uchumi hasa ujenzi wa miundombinu bora ambayo ni nguzo kuu katika kujenga wa uchumi wa viwanda.
Miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sasa kupitia ufadhili wa Benki ya AfDB imefikia zaidi ya dola za Marekani bilioni mbili ambapo uwekezaji mkubwa uko katika sekta za nishati ya umeme, usafiri, miundombinu ya barabara, kilimo, maji na usafi wa mazingira, kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina, mwishoni mwa mwezi uliopita alitembelea kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, mkoani Dodoma, mradi ambao unafadhiliwa na AfDB.
Akiwa katika kituo hicho, Dkt. Adesina alisema benki hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati hapa nchini kwani inachochea mageuzi katika maisha ya wananchi.
“AfDB inatambua na kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kusukuma mbele kurudumu la maendeleo,” alibainisha Adesina.
Aidha hivi karibuni Rais Magufuli alizindua barabara ya Babati-Dodoma kupitia Kondoa yenye urefu wa km 251 iliyojengwa kwa jumla ya shilingi bilioni 378.4 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania (bil. 107.6), AfDB (bil. 203.1) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan-JICA (bil. 67.6).
Katika uzinduzi huo Rais wa AfDB alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake makini na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania katika harakati za maendeleo.
“Hapana shaka kwamba Tanzania sasa ipo kwenye mwelekeo sahihi, nakupongeza wewe binafsi kwa uongozi makini kwani hujabadilika katika utendaji kazi wako tangu ukiwa Waziri wa Ujenzi hadi sasa,” alisema Adesina.
Pamoja na hayo, mashirika mengine ya kimataifa kama Global Fund nayo kwa kuona jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, yamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kuleta maendeleo ya Tanzania hasa katika sekta ya afya.
Global Fund wameendelea kuisaidia Serikali kupitia programu mbalimbali za kuboresha afya za watanzania ikiwemo kupambana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na Ukimwi.
Aidha, nchi mbalimbali barani Afrika pia zinathibitisha uongozi bora wa Rais Magufuli kwa kufuata nyayo zake na kuiga mbinu zake za uongozi katika nchi zao kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Ulinzi na usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi yetu hususan madini, limekuwa ni jambo la mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika.
Zambia mwaka huu imefuata nyayo za Rais Magufuli kwa kudai kodi kiasi cha dola bilioni nane kutoka kampuni moja ya uchimbaji madini ya Canada wakati Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila naye ametia saini sheria mpya ya madini.
Pia viongozi kutoka nchi jirani wamebainisha uongozi bora wa Rais Magufuli kwa kupongeza jitihada zake za kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kwa kasi.
Akizungumza katika hotuba yake hivi karibuni Mkoani Dodoma wakati Rais Magufuli akifungua mkutano wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Spika wa Bunge hilo Martin Ngoga kutoka Uganda alipongeza juhudi za Rais katika kusimamia kwa vitendo dhana ya uchapakazi na uwajibikaji mambo ambayo yameleta ufanisi mkubwa katika shughuli za Serikali.
“Nakupongeza kwa jitihada zako za kupambana na rushwa na ufisadi kwani zimeleta mafanikio makubwa hasa katika utoaji wa haki na kuimarisha utawala bora,” alisema Ngoga.
Aidha katika Bunge hilo Mbunge kutoka nchini Uganda Dennis Namara alisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi bora anayethibitisha uongozi wake kwa vitendo.
“Some men are born great, others achieve greatness and others collide with greatness, Your Excellency indeed you were born great and you have achieved greatness,” Namara alimwagia sifa Rais Magufuli kutokana na namna anavyoingoza Tanzania na kumfanya kuwa wa mfano wa kipekee duniani.
Si hayo tu, yapo mengi ya kueleza na kuthibitisha uongozi thabiti na uzalendo wa Rais John Magufuli katika kuhakikisha nchi yetu inafikia maendeleo ya kweli na kuwa mfano wa kuigwa duniani kote.