Na: Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu katika mkoa wa Pwani kuanzia kesho tarehe 20 Juni 2017 ambapo atazindua miradi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, katika ziara hiyo Rais Dkt. Magufuli atazindua viwanda vikubwa vitano ambavyo ni pamoja na kiwanda cha vifungashio (Global Packaging Co. Ltd), kiwanda cha matrekta (Ursus-TAMCO Co. Ltd), kiwanda cha chuma (Kiluwa Steel Group), kiwanda cha kukausha matunda (Elven Agric Company) pamoja na kiwanda cha vinywaji baridi (Sayona Fruits).
Aidha Rais Magufuli atazindua rasmi mradi wa maji wa Ruvu na Barabara ya Bagamoyo Msata.
Wakati huohuo Rais Dkt. John Pombe Magufuli atatumia ziara hiyo kuzungumza na wananchi wa mkoa wa Pwani ili kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.